Uchunguzi juu ya mchakato wa kubadili mfumo wa uendeshaji (Transformation) wa klabu ya Simba kutoka wanachama kwenda kwenye hisa chini ya Kampuni.
(Imetolewa chini ya Kanuni ya 10 (9) ya Kanuni za Ushindani za Mwaka 2018)
Tume ya Ushindani (Tume au FCC) ni Taasisi ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa sheria ya Ushindani, Namba 8 ya Mwaka 2003 (Sheria ya Ushindani), ili kushajiisha na kulinda ushindani wa biashara na kuwalinda walaji dhidi ya mienendo isiyo ya haki na ya kupotosha.
Tume inapenda kuufahamisha wadau wa michezo na umma wa Watanzania kuwa imefuatilia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Klabu ya Simba Bw. Haji Manara kwenye mitandao ya kijamii pamoja na gazeti la Mwanaspoti la Alhamisi tarehe 24 Septemba 2020 lenye kichwa cha Habari ”Manara: Nitamshangaa Mo Dewji asipoweka pesa.” Taarifa hiyo ilisema pamoja na mambo mengine, kwamba FCC inachelewesha mchakato wa uwekezaji ndani ya Timu ya Simba (trasformation). Aidha, Tume ilifuatilia pia taarifa ya Bw. Mohamed Dewji alipokuwa akiongea na vyombo vy a habari tarehe 15 Novemba 2020, na kusema kwamba mchakato umekwama FCC.
3. Hata hivyo, katika ufuatiliaji wake wa Sports Club (Klabu ya Simba) inaongozwa na Simba Sports Club Company Limited chini ya uenyekiti wa Bw. Mohamed Dewji kabla ya wadaawa hawajawasilisha maombi yao ya muungano (merger application) mbele ya Tume. Kitendo hiki, kwa mujibu wa mwenendo wa uchunguzi wa masuala ya ushindani ni kiashiria cha uvunjifu wa Kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Ushindani. Hivyo, mnamo tarehe 23 Januari
2020, Tume ilianzisha uchunguzi (investigation) juu ya jambo hili kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani;
4. Wakati uchunguzi unaendelea, mnamo tarehe 23 Julai 2020, Tume ilipokea maombi ya muungano wa makampuni (merger application) kutoka kwa wadaawa, wakiijulisha Tume nia yao ya kuichukua Klabu ya Simba na kuiendesha kama kampuni chini ya kampuni mpya waliyoianzisha ya Simba Sports Club Company Limited;
5. Tume iliyafanyia uchambuzi wa awali maombi hayo na mnamo tarehe 30 Julai 2020, Tume iliwajulisha wadaawa kwamba taarifa walizoziwasilisha mbele ya Tume hazikukidhi matakwa ya Sheria ya Ushindani na hivyo kuwataka wawasilishe taarifa husika ili mchakato wa uchambuzi uendelee;
6. Mnamo tarehe 13 Oktoba 2020, Tume ilisitisha kwa muda mchakato wa uchambuzi wa maombi ya muungano wa kampuni (merger application) na kuwajulisha wadaawa. Madhumuni ya kusitisha huko ni kupata taarifa na ufafanuzi zaidi toka kwa wadaawa na wadau wengine. Kwa mfano, taarifa zilizoombwa na Tume kutoka kwa uongozi wa Klabu ya Simba ni pamoja na (a) ufafanuzi kuhusu uteuzi wa Mtendaji Mkuu (Chief Executive Officer) wa Klabu ya Simba kabla ya uwekezaji kufanyika; (b) kiasi halisi ambacho mwekezaji, Bw. Mohamed Dewji anatakiwa kuwekeza ili kuondokana na mkanganyiko ulioko kati ya kiasi kilichotajwa kwenye Mkataba wa Makubaliano
(Memorandum of Understanding) na kile kinachotajwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari;
7. Hadi tarehe 18 Novemba 2020, Uongozi wa Klabu ya Simba haujakamilisha uwasilishaji wa taarifa, nyaraka pamoja na ufafanuzi wa masuala hayo na mengine kadha wa kadha;
8. Tume inapenda kuutaarifu umma kuwa ucheleweshwaji wa mchakato (transformation) wa kubadili mfumo wa uendeshaji wa Klabu ya Simba unatokana na mwitikio hafifu wa kampuni ya Simba Sports Club Company Limited wa kuwasilisha taarifa kamilifu na kwa wakati mbele ya Tume katika kufanikisha uchunguzi tajwa hapo juu.
9. Tume haihusiki na ucheleweshwaji wa mchakato kama ilivyoelezwa na viongozi wa Timu ya Simba hapo juu bali inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
TUME YA USHINDANI
18 Novemba 2020