Dar es Salaam. Sare ya tatu mfululizo ambayo Yanga imepata inawapa ahueni mabingwa watetezi, Simba kujipanga katika mechi zake zijazo za mbio za ubingwa soka nchini.
Yanga, ambayo ilikuwa imeiacha Simba kwa zaidi ya pointi saba ilipopoteza mechi mbili mfululizo, ilijikuta ikilazimishwa suluhu na Gwambina jijini Mwanza, ikatoka sare nyingine ya bao 1-1 na Simba na sare kama hiyo juzi dhidi ya Namungo.
Simba ilifanikiwa kurudi kwa kasi baada ya kushinda mfululizo kabkla ya sare dhidi ya Yanga na baadaye kuirarua Coastal Union mabao 7-0 Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Katika mchezo wa juzi, Yanga ilionyesha kiwango kisichoridhisha huku safu yake ya ulinzi ikishindwa kuelewana na kufanya makosa ambayo hata hivyo Namungo walishindwa kuyatumia.
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ amesema mfumo wa kocha Cedrick Kaze wa kuchezea mpira ni mzuri, lakini anatakiwa kuongeza mshambuliaji.
Kocha Mohammed Adolph Rishard aliisifu Yanga kuwa kwa siku za karibuni imekuwa ikicheza vizuri lakini tatizo lao kubwa ni umaliziaji kwa ajili ya kumaliza mchezo.