Dar es Salaam. Wakati Abdulrazq Mbwana mmoja wa wanafunzi watatu waliofariki baada ya ukuta wa nyumba jirani kuliangukia darasa la Shule ya Chekechea yaJoy Unit Daycare akizikwa jana, baba yake mkubwa amesema siku ya ajali mtoto aligoma kwenda shuleni.
Wakati Abdulrazaq akizikwa, mwili wa mwanafunzi mwenzake, Blaston Gedi umesafirishwa kwenda Iringa kuzikwa huku Neema Nelson akizikwa leo jijini hapa.
Watatu hao walipoteza maisha Jumatano ya Novemba 19. Baba mkubwa wa Abdulrazaq, Jamuhuri Omary alisema alipoamshwa kwenda shule mtoto huyo aligoma akisema mvua itanyesha.
“Aligoma kwenda shule kwa sababu siku moja kabla ya tukio alizuiliwa na mama yake asiende kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha, akamuambia kwa sababu jana hukwenda leo uende mtoto akawa hataki lakini walimlazimisha. Hawakujua kama mauti yangemkuta,” alisema Omary.
Kutokana na tukio hilo, tayari Serikali imekifunga kituo cha Joy Unit Daycare. Licha ya mmiliki wa kituo hicho kuishi hapo lakini jana palikuwa kimya, hakuna aliyeonekana.
Mwenyikiti wa Mtaa Kisiwani, Peter Mwasingi alisema kuanzia Jumatatu ijayo, watafanya ukaguzi wa vituo tisa vilivyopo eneo hilo kuhakikisha kilichotokea hakijirudii kwa kuangalia usalama wa majengo na maeneo yanayozunguka vituo hivyo.
Wakati wazazi wa watoto walionusurika kwenye ajali hiyo wakisema hawatowaruhusu waendelee na masomo, Wizara ya Afya, Jinsia na Watoto inayohusika na usajili wa vituo hivyo imesema imechukua hatua.
“Wanaohusika huko chini wanalishughulikia hili na tusibaki tu Bonyokwa tuliangalie kwa nchi nzimakwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara,” alisema kamishna wa ustawi wa jamii, Dk Naftali Ng’ondi.
Kulingana na takwimu zilizopo, kamishna huyo alisema zaidi ya vituo 1,500 vya kulelea watoto vina usajili wa kudumu na vinatakiwa kuwa na hatimiliki au mkataba wa kukodishiwa eneo.
Kupata usajili huo, alisema mwombaji anahitaji kuwa na uthibitisho wa polisi kwamba hana rekodi ya uhalifu, wadhamini watatu, kipato cha kuendesha kituo, watumishi wenye uwezo kulingana na idadi ya watoto wanaojumuisha mhudumu wa ofisi, mpishi na msaidizi wa watoto.
Pia mwombaji atahitaji barua ya mtendaji kuthibitisha anazo sifa na baada ya hapo ofisa ustawi atakagua vigezo vya eneo la kituo wakati bwana afya atakagua usafi wa mazingira kama yanafaa kwa watoto na eneo halitakiwi kuwa jirani na soko au baa.
“Baada ya kuanzishwa huwa tunafanya ukaguzi wa kushtukiza katika vituo hivyo na kila baada ya robo mwaka hukaguliwa na maofisa ustawi wa jamii na vituo hivi huwa vinapaswa kututumia taarifa ya utendaji kazi wao,” aliongeza Dk Ng’ondi.
VIDEO: