WABUNGE 19 wa Viti Maalum kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Halima Mdee, wameapishwa leo katika viwanja vya Bunge na Spika Job Ndugai jijini Dodoma.
Wengine ni Esther Bulaya, Secilia Pareso, Hawa Mwaifunga, Kunti Majala, Ester Matiko, Sophia Mwakagenda, Naghenjwa Kaboyoka, Salome Makamba, Grace Tendega.
“Nashukuru chama changu (Chadema) kwa kutupa nafasi hii, nafasi hizi siyo hisani bali ni matakwa ya kisheria kutokana na chama chetu (Chadema) kukidhi matakwa hayo,” alisema Halima Mdee kwa niaba ya wenzake na kuongeza:
“Tuwahikikishie wanachama wetu wa Chadema kuwa tutafanya kazi waliyotutuma kwa uadilifu na uaminifu mkubwa sana. Pia nikishukuru chama changu (Chadema), kwani kupitia chama tumepata nafasi hizi.”
Naye Ndugai amesema: “Kwa mujibu wa taarifa niliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), 20 Novemba 2020, nimepokea majina 19 ya wabunge wa Chadema walioteuliwa na NEC na mimi nimewaapisha kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
“Moja ya majukumu ya Spika wa bunge ni kuwalinda wale walio wachache; nitawalinda na kuwapigania ili muweze kutimiza majukumu yenu ya kibunge.”