KESHO timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina kibarua cha kusaka pointi tatu kwenye mchezo wa kufuzu Afcon 2021 dhidi ya Tunisia.
Stars ikiwa kundi J ina kibarua cha kupindua meza kibabe kwa kuwa mchezo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 nchini Sudan.
Tayari wameshaanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa huku Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije akiweka wazi kuwa watatumia faida ya uwanja wa nyumbani kusaka matokeo.
"Tutakuwa nyumbani na nina amini kwamba utakuwa ni mchezo wenye ushindani lakini tupo tayari kufanya vizuri hivyo mashabiki watupe sapoti," amesema.
Kwenye kundi J ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi tatu, imeshinda mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja inakutana na vinara wa kundi hilo ambao wana pointi tisa kibindoni.
Ili kufufua matumaini ya kuweza kufuzu Afcon ni lazima ishinde kesho ili kuongeza mtaji wa pointi kibindoni.
Mchezo wa kesho mashabiki wataruhusiwa kuingia ila sio kwa kiwango kikubwa kwa kuwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limetoa muongozo kwa kuruhusu asilimia 50 ya mashabiki kuingia kutokana na kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.