Mkutano wa kilele wa kundi la mataifa yaliyoendelea na yale yanayoinukia kiuchumi G20 unaanza leo chini ya mwenyeji Saudi Arabia, ukigubikwa hata hivyo na kiwingu cha janga la virusi vya corona.
Shughuli za mkutano huo wa kilele ambao kwa kawaida huwakutanisha ana kwa ana viongozi wa madola yenye nguvu zimepunguzwa na badala yake kutakuwa na majadiliano mafupi kupitia njia ya video kuhusu masuala tete yanayoukabili ulimwengu hususan athari za janga la virusi vya corona.
Rais Donald Trump wa Marekani atashiriki mkutano huo utakaojadilia pia suala la mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa duniani.
Kulingana na rasimu ya taarifa ya pamoja itakayotolewa na viongozi watakaohudhuria, kundi la G20 litaahidi kufanya kila linalowezekana kudhibiti kusambaa janga la COVID-19 na kufufua uchumi wa ulimwengu.