Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, amesema kuwa sasa hivi suala la uchaguzi limekwisha na kilichopo kwa sasa ni kujenga na kutengeneza maendeleo ya Taifa hilo.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 5, 2020, jijini Dodoma, wakati akihutubia Watanzania mara baada ya kula kiapo cha kuliongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mitano ijayo.
"Uchaguzi sasa umekwisha, jukumu kubwa lililopo mbele yetu ni kuendeleza jitihada za kujenga na kuleta maendeleo kwa Taifa letu na niwahakikishie kuwa kiapo nilichoapa na alichoapa makamu wangu tutahakikisha na kukienzi kwa nguvu zote", amesema Rais Magufuli,
Awali akihutubia Rais Magufuli amesema kuwa, "Niwashukuru na kuwapongeza Watanzania kwa kuonesha utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi, kama mjuavyo kwenye baadhi ya nchi uchaguzi umekuwa chanzo cha uhasama, sisi Watanzania tumevuka mtihani huo salama na kuthibistha ulimwengu sisi ni wapenda amani".