Viongozi wengi duniani kote wamempongeza Rais mteule wa Marekani Joe Biden kwa ushindi wake, wakishangilia fursa ya kuimarisha demokrasia ya ulimwengu pamoja na taifa hilo kupata makamu wa rais wa kwanza wa kike.
Ingawa Rais Donald Trump bado hakukubali kushindwa, katika sehemu nyingi za ulimwengu watu wengi wamefurahia kushindwa kwake kuchaguliwa tena urais.
Mataifa mengi ya magharibi yamempongeza Biden, na kuonyesha utayari wao wa kuanza kufanya kazi kwa ushirikiano na utawala mpya wa Marekani.
Salamu za pongezi zimepokelewa kutoka kwa viongozi wa mataifa ambayo hayakukubaliana na sera za utawala wa Trump, lakini vile vile kutoka kwa viongozi ambao walikuwa na wameelewano mazuri na Trump na kuamua kupuuza madai yake kwamba mchuano huo bado haukumalizika.