Wakati bondia Jose Carlos Paz kutoka Argentina anawasili leo, mpinzani wake Hassan Mwakinyo amebadili ratiba ya mazoezi na sasa anajifua masaa manne kwa siku.
Mwakinyo ameweka kambi eneo la Magoroto, Muheza mkoani Tanga kuelekea pambano la kutetea ubingwa wa mabara wa WBF na kuwania ubingwa mpya wa mabara wa IBA wa uzito wa super-welter.
Bondia huyo anajifua chini ya kocha, Hamis Mwakinyo pamoja na wasaidizi mbalimbali huku wakitumia video mmbalimbali kumsoma Paz ambaye ana rekodi nzuri.
“Nimehama nyumbani na kujichimbia huku Magoroto kwa lengo la kufanya vyema katika pambano hilo, kujifua zaidi ya raundi 12 ili kupata stamina ya kwenda sambamba na mpinzani wangu,” alisema Mwakinyo.
Katika hatua nyingine, waandaaji wa pambano hilo wamesema kuwa tiketi kwa ajili ya pambano hilo zitauzwa mtandaano kupitia kampuni za Nilipe na Selcom.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jackson Group Sports Kelvin Twissa alisema kuwa viingilio kwa pambano hilo vitaanzia Sh150,000 kwa eneo la kawaida na meza ya watu 10 itauzwa kwa sh milioni 3 ambao watapata huduma mbalimbali zilizoandaliwa.
Twissa alisema kuwa mbali ya Mwakinyo na Paz, pia siku hiyo kutakuwa na pambano makali ambapo bondia nyota wa kike, Zulfa Macho atazipiga na Alice Mbewe kutoka Zambia wakati Hussein Itaba atazichapa na Alex Kabangu katika uzito wa super-middle.
Siku iyo pia bondia nyota kutoka Kenya, Fatuma Zarika atazichapa na Patience mastara wa Zimbawe katika uzito wa super bantam.
Wakati huo huo; mpinzani wa Mwakinyo, Paz ameamua kuwasili mapema Tanzania ili kuzoea hali ya hewa.
Paz anatarajiwa kuwasili usiku huu saa 4.30 kwa ndege ya KLM na msafara wake utaambatana na kocha wake, Oscar Alberto Ramon.
Mwakinyo akijifua kuelekea pambano dhidi ya Muargentina Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oysterbay.