Vyombo vya habari vya kibinafsi nchini Uganda, vimekataa kupeperusha hotuba ya rais Yoweri Museveni ambayo alikuwa amepanga kufanya kila Jumapili, kuanzia saa moja kamili jioni hadi saa tatu usiku saa za Kampala.
Museveni alikuwa ameagiza vyombo vyote vya habari nchini Uganda kupeperusha hotuba yake ya kila wiki, lakini muungano wa wamiliki wa vyombo hivyo umekataa agizo hilo wakisema huu ni msimu wa kampeni na kwamba hawawezi kutoa fursa kwa mgombea mmoja pekee bila kuzingatia wagombea wengine kwa sababu inavunja kanuni za uandishi wa habari.
Taarifa ya muungano wa wamiliki wa vyombi vya habari Uganda umeandikia tume ya mawasiliano Uganda – UCC, ukisema kwamba “Museveni ni mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu mwa mwaka 2021 na kwa hivyo tukipeperusha hotuba yake, wasikilizaji na watazamaji watachukulia ujumbe wake kama kampeni.”
Ameandika katibu wa muungano huo Joseph Beyanga. Kulingana na sheria ya utangazaji nchini Uganda ya mwaka 2013, kila mgombea katika uchaguzi anastahili kupewa nafasi sawa katika vipindi na habari zinazochapishwa au kupeperushwa na vyombo vyote vya habari nchini humo. Kulingana na msemaji wa Museveni, Don Wanyama, hotuba ya Museveni ya jumapili ilikuwa imepangiwa kuangazia usalama na ukuaji wa uchumi.
Baada ya muungano wa vyombo vya habari kukataa kupeperusha hotuba hiyo, Wanyama aliandika ujumbe wa twitter kwamba “hotuba ya rais imeahirishwa hadi siku ambayo tutawaarifu. Tunasikitika kwa usmbufu wowote ambao umejitokeza.” “Tungependa kujua aina ya hotuba atakayotoa rais Museveni kabla ya kupanga namna ya kuipeperusha. Iwapo hotuba hiyo ni kampeni, basi vyombo vya habari vinavyotaka kuipeperushwa vinastahili kulipwa kwanza.” Imesema barua ya muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari kwa mamalaka ya mawasiliano UCC. Maafisa wa UCC hawajajibu barua hiyo. Museveni mwenye umri wa miaka 76, anagombea mhula wa sita madarakani kupitia chama cha National resistance movement NRM.
Machafuko yalitokea Uganda wiki iliyopita baada ya polisi kukamata mgombea wa urais wa chama cha National unity platform – NUP, Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, kukamatwa na maafisa wa polisi.
Alifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kufanya kampeni katika njia inayoweza kusambaza virusi vya Corona.
Aliachiliwa kwa dhamana na anaendelea na kampeni yake. Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC