Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi wameeleza mtihani inaokipitia chama cha ACT- Wazalendo kuhusu kujiunga au kutojiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) wakishauri pande mbili ziafikiane.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, chama kinachoruhusiwa kutoa Makamu wa kwanza wa Rais ni lazima kiwe na zaidi ya asilimia 10 ya kura za urais. Mgombea urais wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad alipata zaidi ya asilimia 19 ya kura akimfuatia Rais Hussein Mwinyi aliyepata zaidi ya asilimia 76.
Hata hivyo, ACT- Wazalendo imekuwa ikilalamikia mwenendo wa uchaguzi huo ikisema kuwa ulivurugwa na kwamba baadhi ya wanachama wake wameuawa, kujeruhiwa na wengine wamekimbia makazi yao.
“Wanatakiwa watafakari manufaa ya kuingia au madhara ya kutoingia kwenye serikali hiyo,” alisema Awadhi Said, ambaye ni mwanasheria maarufu wa Zanzibar.
Aliendelea: “Kwa sasa wako njia panda kwa sababu wanalalamikia uchaguzi mkuu wakisema ulivurugwa. CCM imepata majimbo 14 kati ya majimbo 18 kisiwani Pemba, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa. Halafu ACT haijapata hata jimbo moja Unguja wakati ina ngome zake. Haijawahi kutokea.
“Haya matokeo hayana uhalisia wa hali ya siasa za Zanzibar. Halafu ACT Wazalendo wana malalamiko, wanadai watu wao wameuawa, wengine wamejeruhiwa na wengine wamekimbia nyumba zao. Kuingia kwenye serikali hiyo itakuwa sawa na kuhalalisha hayo malalamiko.”
Hata hivyo, alisema chama hicho kinaweza kuingia kwenye Serikali hiyo kwa kuwa Dk Mwinyi ni Rais mpya huku akiwa hana mizizi kwa siasa za Zanzibar.
“Wasipoingia maana yake watakuwa nje ya mfumo, labda kwa kuwa rais huyu ni mpya na hana rekodi za siasa chafu visiwani wanaweza kuingia,” alisema Awadhi.
Maoni hayo yameungwa mkono na Profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mohamed Bakari wa aliyesema ACT -Wazalendo wanapaswa kutafakari ili wasijishushie heshima yao kisiasa.
“Inabidi wafanye cost benefit analysis (uchambuzi wa gharama na faida) ya ama kushiriki au kutoshiriki kwa sababu kila upande una faida na hasara.
“Kama ni kushiriki watakuwa wanahalalisha kile wanachodai kuwa uchaguzi ulivurugwa na watakuwa wanawasaliti wafuasi wao,” alisema.
Hata hivyo, alisema kushiriki kwa ACT Wazalendo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa hakuna faida kubwa, kwa kuwa nafasi mbili za uwaziri hazina nguvu za kupinga uamuzi utakaotolewa na upande wa CCM.
“Kwanza hiyo nafasi ya Makamu wa kwanza wa urais haina nguvu kubwa kimaamuzi, ni kama pambo tu, hilo pia inabidi liangaliwe. Hata hizo nafasi mbili za uwaziri hazina nguvu kubwa.
Msomi mwingine, Dk George Kahangwa ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema pamoja na Serikali kuiandikia barua ACT Wazalendo, bado Rais Mwinyi ana jukumu la kukutana na viongozi wa chama hicho.
“Barua peke yake haitoshi, ni vyema Dk Mwinyi akaitisha meza ya mazungumzo na ACT-Wazalendo ili kuondoa hali ya hewa iliyopo. Rais huyu mpya ana wajibu wa kujenga mshikamano na ushirikiano kwa Wazanzibar wote,” alisema Dk Kahangwa.
Mchambuzi wa siasa Zanzibar , Profesa Ali Makame Ussi alisema kitendo cha ACT kuchelewesha wawakilishi wake kwenda kuapishwa kinachelewesha maendeleo.
“Hali hii imetuacha katika nafasi ambayo tunaendelea kujiuliza kama suala hili linaweza kutokea haraka au tusubirie,” alisema.
Wapongeza muundo wa Baraza
Wakati huohuo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wameonyesha matumaini yao ya Zanzibar kuimarika kiuchumi kutokana na baraza imara lililotangazwa na Dk Mwinyi.
Hassan Khamis, mkazi wa Fuoni alisema sura mpya nyingi katika baraza hilo ni ishara mojawapo ya kila mmoja kuwa na shauku ya kufanya kazi.
“Naamini kwa kuwa mawaziri wengi ni wapya, kasi anayohitaji rais wetu ya ukuaji uchumi inaweza kufikika, kutokana na kila mmoja kuonekana ni mtendaji bora,”alisema.
Naye mkazi wa Pangawe, Faki Ame, alisema uaminifu ni mojawapo ya sifa zilizomsukuma Dk Mwinyi kuwateua viongozi hao, hivyo ni matumaini ya wanachi kwamba kasi ya maendeleo inaweza kufikika kwa muda mfupi.
“Jambo la msingi ni kwa wateule hao kuwa na uzalendo wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao ya uwaziri, bila ya kuwabagua wananchi wanaowategemea,” alisema