Walichosema Halima Mdee Mdee, Matiko baada ya kuapishwa Bungeni




 Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Halima Mdee amewaahidi wanachama wa chama hicho kuwa wanakwenda bungeni kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu.
Mdee amezungumza kwa niaba ya wabunge wenzake 19 walioapishwa na Spika Job Ndugai leo Jumanne tarehe 24 Novemba 2020, Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
 

Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) ameanza kwa kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufikia siku ya leo pamoja na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe.

“Tunakishukuru chama chetu Chadema kikiongozwa na Freeman Mbowe kwa kupitia wao, tumepata nafasi hii ya kukiwakilisha chama chetu,” amesema Mdee, aliyewahi kuwa mbunge wa Kawe kati ya mwaka 2010-2020.

“Tutafanya kazi kwa uaminifu kama kambi ya upinzani bungeni kwa viwango vilevile. Tunawahakikishia Chadema nchi nzima, tutafanya kazi mliyotutuma na kwa uadilifu mkubwa sana,” amesema

Kwa upande wake, Spika Ndugai amesema, tarehe 20 Novemba 2020, alipokea barua kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikimjulisha uteuzi wa wabunge hao 19 wa viti maalum.

“Nawapongeza sana na kuwatakia kila la kheri katika safari yenu ya miaka mitano. Mimi kama spika, nawaahidi kuwapa kila ushirikiano, nitawalinda na kuwapa haki kikamilifu,” amesema Spika Ndugai

Matiko amesema, “kuna utaratibu uliendelea ndani ya chama, kisha majina yakapelekwa tume na mimi nikateuliwa.”

“Tuko 19, yaliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu kila mtu anajua, tutatumia uchache wetu kutetea maslahi ya chama na Watanzania. Tunakishuruku chama chetu kwa kututeua,” amesema

Hata hivyo, baadhi ya maswali aliyoulizwa na waandishi juu ya mkanganyiko ya kimsimamo kuhusu kutoshiriki ndani ya Bunge amesema, “leo ilikuwa kazi ya kuapa, mimi si msemaji wa chama, kama kutakuwa na mengine tutazungumza.”

Mapema leo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alitumia ukurasa wake wa Twitter kuzungumza suala hilo, akisema hafahamu lolote na chama hicho, hakijateua jina lolote.

“Niliandika barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kuwajulisha. Tunafuatilia yanayojiri Ofisi ya Spika wa Bunge na tukithibitisha hujuma au usaliti hatutasita kuchukua hatua,” alisema Mnyika


Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hongereni Wabunge wateule Kina Mama.

    Kachapeni Kazi, Kweli Kweli.

    Wacheleweshaji,waachieni na yao njiani

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad