Wanaotuhumiwa Kuvujisha Mitihani Wapelekwa Takukuru

  


Arusha. Walimu waliotajwa kuhusika na udanganyifu katika mitihani ya darasa la saba katika jiji la Arusha na Wilaya ya Kiteto, mashauri yao wamepelekwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru)


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde akitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba wiki iliyopita, alizitaja shule za msingi Dominion ya Arusha na Olkitikiti ya wilaya ya Kiteto kuwa ni kati ya shule 38 ambazo watahiniwa wake 1,059 walifutiwa matokeo kutokana na udanganyifu.


Alisema katika shule ya Dominion mwalimu wa shule hiyo, Shamsidini Ahmed alikamatwa akiwa amejificha chooni akiwapatia watahiniwa vikaratasi vyenye majibu ya mtihani wa somo la Social Studies na katika purukushani alitupa chooni majibu hayo.


Tayari shauri la mwalimu Ahmed limefikishwa Takukuru na vyombo vingine vya sheria kwa uchunguzi zaidi.


Katika shule ya Olkitikiti ilibanika Seremon Sanaki aliyemaliza darasa la saba mwaka 2019 akimfanyia mtihani Ngushani Seuru na Oleserian Rokoine mwanafunzi wa darasa la sita akimfanyia mtihani Orkianga Masinyai.


Pia mwalimu mkuu wa shule hiyo, Oscar Waluye alibanika kutafuta watu kuwafanyia mitihani watoto watoro ili shule yake isiwe na watoro na wote walikamatwa.


Ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Kiteto, Emmanuel Mwagala alisema baada ya Takukuru kumkamata mwalimu aliyekuwa akifanya udanganyifu wameamua sheria ifuate mkondo wake.


“Tutachukua hatua za kinidhamu kwa mwalimu, lakini kwa sasa Takukuru wanaendelea naye kisheria kwa kuwa ndio waliokuwa wamemkamata”alisema.


Mkuu wa Takukuru wilaya, Venance Sangau akizungumzia sakata hilo alisema mwalimu huyo bado hajapelekwa mahakamani ila taratibu zinaendelea.


Mkuu wa wilaya Kiteto Kanali Patrick Songea kufuatia mwalimu huyo kuingiza mamluki darasani kuwafanyia wanafunzi wadiojiweza alisema sheria itafuata mkondo wake

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad