Wapinzani watoa ya moyoni hotuba ya Rais Magufuli bungeni

 


By Elias Msuya na Fortune Francis, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hotuba ya Rais John Magufuli wakati akizindua Bunge la 12, inaweza kuwa ilijaa maelezo ya kina kuhusu mipango ya Serikali yake katika miaka mitano ijayo, lakini sifa alizoipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zimepingwa na viongozi wa vyama vya siasa.


Baadhi wametaka kuwapo kwa meza ya mazungumzo kutibu majeraha ambayo wanasema yamesababishwa na NEC na Jeshi la Polisi, na wengine kuahidi kuendeleza mapambano ndani na nje ya nchi, huku wengine wakiwa hawaelewi mustakabali wa shughuli za kisiasa baada ya Rais kusema “uchaguzi umekwisha”.


Akizungumza wakati wa kuzindua Novemba 13, Rais Magufuli alisema uchaguzi huo wa Oktoba 28 ulifanyika kwa uwazi, amani na utulivu mkubwa.


“Kwa msingi huo napenda nirudie kupongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusimamia vizuri uchaguzi mkuu mwaka huu; kuanzia uandikishaji wapigakura, uchukuaji na urejeshaji fomu za wagombea, usimamizi wa kampeni, upigaji kura na utoaji wa matokeo mapema,” alisema Rais akilihutubia bunge hilo lenye wabunge wanne tu wa upinzani.


“Kwa hakika tumethibitisha uwezo mkubwa kusimamia uchaguizi bila kutegemea misaada kutoka nje.”


Kauli yake imekuja wakati vyama vya wapinzani na wadau vikilalamikia mawakala wao kuzuiwa kuingia vituoni, kukamatwa kwa kura feki na kuenguliwa kwa wagombea wao.


Vyama vya Chadema na ACT- Wazalendo vilitangaza maandamano ya kupinga matokeo hayo, lakini viongozi wake wakakamatwa usiku wa kuamkia siku ya maandamano.


Hata hivyo, wakati vyama hivyo viwili vikubwa vya upinzani vikipinga matokeo, AAFP, Demokrasia Makini, DP, UPDP, SAU, NRA, ADC, UMD na NCCR-Mageuzi vilivyosimamisha pia wagombea urais, vilitangaza kumuunga mkono Rais Magufuli.


Jana, mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema kuna maumivu ambayo yamesababishwa na NEC kwa kushirikiana na vyombo vya dola, hali ambayo alisema imeirudisha nchi nyuma kwa miaka 28, akirejea mwaka 1992 ambao siasa za ushindani zilirejeshwa nchini.


Alisema ili kutibu majeraha hayo kunahitajika mazungumzo ya pamoja, akisema Rais anapaswa kusikiliza sauti za wasioridhishwa na uchaguzi huo.


“Tanzania imekuwa kinara wa kuhakikisha kuwa nchi zinakuwa na amani, kwa hiyo duniani inayozungumzwa ni meza ya mazungumzo, meza ya mazungumzo,” alisema Mbatia baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu mahojiano yake na BBC.


“Mtu asiyetaka kuliona hilo kwa kweli ajue kwamba tunarudi nyuma. Naona kuna giza nene mbele yetu. Tanzania ni mali ya Watanzania wote, ikiharibika tunaharibikiwa sote. Sasa tukubaliane kuwa kuna tatizo. Ninaamini itafika mahali kwa sababu hii chuki inayoendelea kwa sababu itatumumiza sisi sote.”


Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alisema si jambo jema kuipa sifa NEC kwa kazi iliyoifanya katika uchaguzi, wakati kuna wagombea na vyama havikutendewa haki.


“Si ajabu kwa yeye kusema uchaguzi huu ulikuwa huru na wa haki,” alisema Lissu ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Rais.


“Uchaguzi umesimamiwa na tume ambayo ameiteua yeye mwenyewe, umeendeshwa na wasimamizi wa uchaguzi aliowateua yeye mwenyewe ambao ni wakurugenzi wa halmashauri.


“Uchaguzi uligubikwa na sintofahamu kwa kuwa mawakala wetu walizuiwa kuingia vituoni, wengine walicheleweshwa kuingia na wapo ambao waliingia muda ukiwa umekwenda sana,”alisema.


NEC imekuwa ikilalamikiwa kwa kutumia wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi majimboni, wakati watumishi hao wa umma ni wateule wa Rais ambaye chama chake pia kinasimamisha wagombea.


Alidai kuwa mawakala 57,900 wa Chadema walizuiwa kuingia vituo vya kupiga kura katika majimbo 190 na kwamba waliobaki kama 12,000 walicheleweshwa kuingia vituoni.


“Takribani mawakala 10,000 ndiyo waliingia vituoni. Hao waliocheleweshwa nao hawakukaa mpaka mwisho waliondolewa kabla ya matokeo hayajatangazwa,” alisema.


“Kwa hali ilivyokuwa, tutakachokifanya ni kuongeza mapambano ya kidemokrasia ndani na nje ya nchi kuhakikisha tunatengeneza mfumo wa demokrasia wa kuongoza nchi yetu wa kuhakikisha hakuna Rais anayetawala bila demokrasia.”


Mwingine aliyekosoa sifa hizo ni Naibu katibu mkuu wa ACT Wazalendo, Joran Bashange aliyesema pamoja na chama hicho kutokubaliana na uchaguzi, hotuba ya Rais Magufuli ina upungufu.


Alisema NEC iliyopongezwa ndio inayolalamikiwa na vyama vyote kwa kipindi kirefu kwa kuharibu uchaguzi, akitoa mfano wa suala la kura feki au mawakala kuondolewa vituoni.


“Ukiangalia, ulikuwa ni mpango na mkakati wa Tume,” alisema.


“Hatukubaliani na NEC, hatukubaliani na uchaguzi ukizingatia asilimia 90 ya Bunge ni la chama kimoja. Mipango hiyo ilitumika katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Unawezaje kuipongeza NEC bila kuwa na Tume huru na Katiba mpya?”


Kuhusu hoja ya kuimarisha demokrasia, Bashange alisema Rais Magufuli ameacha alama ya kuuliza kwa kuwa hakufafanua kuhusu mikutano ya hadhara ambayo haikufanyika tangu mwaka 2016 baada ya kupigwa marufuku na Serikali.


“Demokrasia kwao ni uwepo wa vyama vingi visivyokuwa huru,” alisema.


“Na sisi tunafahamu itakuwa tofauti na alivyozungumza ataendeleza mambo yaleyale sisi kwetu hatujaona jambo jipya.”


Kauli hiyo iliungwa mkono na Naibu katibu mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya aliyesema: “Hiyo ni kauli ya ajabu kabisa. Kwa sisi tulioingia katika uchaguzi na kwa hayo tuliyoyaona, kama ni kubakwa kwa demokrasia, basi uchaguzi huu ulikuwa ni wa kubaka demokrasia.”


Sakaya, aliyegombea ubunge wa Kaliua, alisema malalamiko yao yanaendeleza chachu ya kudai mabadiliko ya Katiba na tume huru ya uchaguzi.


“Mimi nimegombea katika jimbo, nimeona kabisa jinsi walivyojipanga kuhakikisha kuwa majimbo yote yanabaki CCM, kata zote CCM na jinsi walivyohakikisha hata watu wanaokosoa, hawawezi kupata fursa ya kukosoa.


“Ndiyo maana tunasema kuna ulazima wa Watanzania tuungane kwa pamoja bila kujali tofauti zetu. Suala la kuwa na Katiba mpya si la kuachia vyama vya siasa, suala la kutokuwa na tume huru ya uchaguzi linaathiri kila mtu,” alisema Sakaya.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad