Watanzania Wanne Wahukumiwa Kenya

 


Moshi. Watanzania watatu kati ya wanne wanashikiliwa nchini Kenya baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh105,000 za Kenya (zaidi ya Sh2.1 milioni) walizotozwa kwa kuingia nchini humo bila kibali wala kuvaa barakoa.


Watu hao ambao ni wafanyabiashara kila mmoja alitozwa faini ya KSh30,000 (Sh600,000) kwa kosa la kuingia nchini humo bila kibali na KSh5,000 (Sh100,000) kwa kutovaa barakoa.


Kati ya wafanyabiashara wanne waliokamatwa Novemba 11 walipokwenda kununua nyanya, ni Wilfred Moshi pekee ndiye alifanikiwa kulipa faini baada ya kuchangiwa na ndugu zake.


Taarifa zinasema wafanyabiashara hao walivuka mpaka kupitia eneo la Kitobo ambako kwa upande wa Kenya kuna mashamba makubwa ya nyanya ili wazilete nchini.


Kamishna msaidizi wa Idara ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro, Edward Mwenda alithibitisha kushikiliwa kwa Watanzania hao akibainisha kuwa hawakuwa na hati za kusafiria.


“Walipita njia za panya na walipokamatwa walitozwa faini ya Sh700,000 kila mmoja ambazo mmoja tu alifanikiwa kulipa,” alisema Mwenda.

 

Mkuu huyo alisema wanafanya mawasiliano na maofisa wa uhamiaji wa Kenya kuona kama mahakama inavyoweza kuwasaidia kupunguza faini hizo maana wenyewe hawana uwezo wa kkulipa.


“Ukipita njia ambazo sio rasmi ukikamatwa sheria zinachukua mkondo wake kama kawaida. Ukitaka kwenda Kenya au kuja Tanzania ndani ya kilometa 10 unaruhusiwa kupita kwa sababu ya ujirani mwema,” alisema.


Moshi, mmoja wa wafanyabiashara waliokamatwa lakini akalipa faini ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Makuyuni alisema “tulienda kuchukua tomato (nyanya) tulipofika tukapigwa stop (kusimamishwa) na askari wa Kenya wakatufunga pingu wakatupeleka polisi wakatuingiza kwenye chumba cha matope.”


Kwenye chumba hicho alisema walikaa kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa saba usiku ndipo walipelekwa ofisi za uhamiaji kabla ya kufikishwa mahakamani kusomewa mashitaka waliyoyakubali kabla hawajahukumiwa kulipa faini au kwenda jela kwa miezi minne

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad