Yanga Yarudi kwa Straika wa Zambia




BAADA ya Yanga kulazimishwa sare ya 1-1 na Namungo, Jumapili iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, imewanyanyua viongozi wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo na kurudi kuiwania saini ya Straika wa Zesco United ya Zambia, Jesse Were raia wa Kenya.

 

Tangu dirisha la usajili lililopita, Yanga walikuwa katika mipango ya kumpata straika huyo ili kutibu tatizo la ushambuliaji kwenye kikosi hicho, lakini dili hilo likafeli.

 

Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimelidokeza Spoti Xtra kuwa, muda wowote Kamati ya Usajili ya Yanga itaenda kukamilisha dili la kumnasa Were ambaye wamekuwa wakimvizia kwa muda mrefu.

 

“Nawashukuru sana viongozi wenzangu kwa kuendelea kuliona tatizo la safu ya ufungaji ndani ya kikosi cha timu yetu, ukiangalia timu yetu imekamilika katika idara ya viungo na ulinzi ila tuna shida katika ufungaji jambo linalotufanya sasa kuangalia zaidi wachezaji wenye kutatua shida hiyo.

 

“Kama unakumbuka vizuri msimu uliopita tulikuwa na mazungumzo ya kina na Zesco United juu ya washambuliaji wao, ambapo tulishindwa kumalizana kutokana na kuwepo kwenye mikataba mirefu, ila sasa tumeweza kufikia makubaliano ambayo yanaenda kumaliza dili hili,” kilisema chanzo hicho.

 

Alipotafutwa Kocha wa Yanga, Cedric Kaze kuzungumzia mipango yake ya usajili, alisema: “Ni ngumu kuzungumzia usajili mpya wa dirisha dogo hivi sasa, kwani hatakama nikiwazungumzia na kuwasajili hatutaweza kuwatumia, hivyo nimeona hilo niliweke pembeni.

 

“Nitaanza kuwazungumzia wachezaji wapya wa kuwasajili baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi kumalizika tena kwa sisi Yanga kuongoza katika msimamo. “Kwani mzunguko huu wa kwanza ndiyo utanipa picha juu ya ubingwa wa ligi msimu huu, malengo yetu kama timu ni kuuchukua kutokana na mipango yetu tuliyokuwa nayo.”

GPL

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad