Uongozi wa mabingwa wa kihistoria wa Tanzania bara Yanga SC, umeeleza kushtushwa na kusikitishwa na tukio la kukamatwa kwa ofisa wao Senzo Mazingiza na kuhojiwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za upangaji matokeo.
Taarifa iliyotolewa na klabu ya Yanga inasema.
“Klabu ya Yanga, imeshitushwa na kusikitishwa na tukio la kushikiliwa na kuhojiwa kwa mmoja wa maofisa wetu katika kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es salaam jana (Novemba 11, 2020) kwa tuhuma za upangaji matokeo. Tukio hili linasikitisha kwani inatoa ishara kwamaba kuna malengo na mipango ovu ya kuichafua klabu yetu pendwa na mfanyakazi wetu lakini pia kuliweka soka la Tanzania katika maswali”
Taarifa hii ya Yanga inafuatia baada ya hapo jana mshauri wa klabu hiyo kwenye mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo Senzo Mazingiza Mbatha kukamatwa na kuhojiwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za upangaji matokeo lakini baadaye aliachiwa.
Novemba 1, 2020, iliripotiwa kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa wanachama wa Simba SC Hashim Mbaga alikamatwa na Polisi kwa kosa la kuihujumu klabu ya Simba ipoteza baadhi ya michezo, na Senzo Mazingiza alitajwa kuwa ni moja ya watu ambao walihusika kwenye mipango hiyo.
Senzo raia wa Afrika Kusini alifanya kazi akiwa Mtendaji mkuu wa Simba SC kati ya Septemba 7, 2019 mpaka Agosti 9, 2020 alipotangaza kujiuzulu na akajiunga na watani zao Yanga SC.
Lakini taarifa hiyo ya Yanga ilisisitiza kuwa inaamini maswala ya mpira wa miguu yanashughulikiwa na taasisi zinazohusika na usimamizi wa mpira wa migiuu na si vinginevyo.