KLABU ya Yanga imewajibu watani wao Simba baada ya kuhamishia ofisi zake Mtaa wa Samora Avenue, Posta jijini Dar es Salaam, badala ya Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyokuwepo mitaa ya Jangwani na Twiga. Simba ndiyo walioanza kuhamishia ofisi zake Posta ambayo yenyewe ipo kwenye Jengo la Golden Jubilee Tower lilikuwepo Mtaa wa Ohio, Dar.
Wakati ofisi zikihamia huko, Jangwani bado iliendelea kuwepo Makao Makuu ya Klabu ambayo bado wapo baadhi ya viongozi wa chini wanaoendelea na kazi kama kawaida. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, shughuli zote za utendaji zinazohusu klabu hiyo na watendaji wa juu zaidi sasa zinafanyika kwenye ofisi hizo mpya zilizopo kwenye jengo hilo jipya lilipo Samora ghorofa ya tisa.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa jengo hilo limekodishwa na wadhamini wa klabu hiyo Kampuni ya GSM, baada ya kuhamisha ofisi zao kutoka Mtaa wa Lumumba, Kariakoo na kuzipeleka kwenye jengo hilo. Aliongeza kuwa lengo la kukaa katika jengo moja ni kufanya kazi za kiutendaji kwa ushirikiano wakati wakiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo mpya wa mabadiliko ya klabu hiyo yanayosimamiwa na La Liga ya nchini Hispania.
“Ninaweza kusema kuwa ofisi za Yanga hivi sasa zimehamia katikati ya mji, Posta kutokana na viongozi wa juu kufanya kazi zote za utendaji huko. “GSM imehamisha ofisi zake zilizokuwa Mtaa wa Lumumba, Kariakoo na kuhamia Mtaa wa Samora Avenue, Posta ambako lipo jengo jipya lililojengwa hivi karibuni,” alisema mtoa taarifa.
Championi hivi karibuni lilishuhudia baadhi ya viongozi wa Yanga na GSM wakiingia kwenye ofisi hizo mpya wakati wakiwa wanakamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji mpya timu hiyo, Mrundi Said Ntibazonkiza.
Wilbert Molandi na Ibrahim Mussa,Dar