WATU wanne ambao ni abiria waliokuwa wakisafiri na basi la Frester lenye namba za usajili T915 CGU kutoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwenda jijini Mwanza, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kumshambulia dereva wa lori, Emmanuel Nobert, wakidai alitaka kuwasababishia ajali.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, amebainisha hayo jana Desemba 23,2020, alipozungumza na waandishi wa habari na kusema katika tukio lilitokea Desemba 21 mwaka huu, katika Kijiji cha Samuye wilayani Shinyanga na kuzagaa mitandaoni likionyesha abiria wa basi wakimshambulia dereva wa lori kwa tuhuma za kutaka kuwasababishia ajali.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Joyce Charles, Athumani Mussa, Christopher Rangati na Mwita Chaguche ambaye ni dereva wa basi la Frester, wote wakishikiliwa kwa tuhuma za kumshambulia na kumpiga Nobert.
“Chanzo cha mkasa huo ni dereva wa basi la Frester kumfanyia vurugu dereva wa lori hilo kwa kuanza kumbana ubavuni ili ampishe awahi kupimwa uzito kwenye mizani ya Tinde, lakini dereva huyo wa lori aligoma na kisha kupimwa gari lake uzito na kuanza kuondoka kwenda jijini Mwanza akitokea Moshi,” amesema Magiligimba.