ACT- Wazalendo yaiionyeshea kidole jeshi la polisi kifo cha kada wake, lenyewe latoa ufafanuzi




Na Ahmad Mmow, Lindi.
Chama cha Alliance for Change and Transparency ( ACT-Wazalendo) mkoa wa Lindi kimelihusisha na kulituhumu jeshi la polisi kifo cha mwenye kiti wa ngome ya wanawake wa ACT- Wazalendo tawi la Kibutuka, wilaya ya Liwale, Aziza Kibou.

Juzi akizungumza na waandishi wa habari mjini Lindi, mwenyekiti wa mkoa wa Lindi wa ACT- Wazalendo, Isihaka Mchinjita alisema kumejitokeza ukiukwaji wa haki za binadamu katika wilaya ya Liwale. Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2020, uliofanyika tarehe 28, mwezi Oktoba.

Alisema kufuatia vitendo vya uchomaji moto majumba na magari vilivyofanywa na baadhi ya wananchi wilayani humo baada ya uchaguzi huo imekuwa ni sababu ya polisi kutimiza wajibu wake wa msingi wa kulinda usalama raia na mali zao kwa kuwasaka wahusika wa vitendo hivyo ili wafikishwe kwenye mikono ya sheria kutumia nguvu kubwa kupita kiasi.

Alisema licha ya chama hicho kutokuwa na kipingamizi na zoezi hilo lakini uendeshaji wake unakiuka kwa kiwango kikubwa haki za binadamu wilayani humo.  Kwani nguvu zinazotumika ni kubwa nakusababisha zoezi hilo ligeuke kuwa utesaji na mauwaji. Kitendo ambacho kimesababisha kada wake, Aziza Kibou(29) kuuwawa bila kosa na kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Mchinjita alisema Aziza ambae alikuwa katibu wa ngome ya wanawake wa ACT- Wazalendo aliuwawa tarehe 28.12.2020 usiku katika kijiji cha Kibutuka kutokana na operesheni hiyo ya polisi. Huku mume wa marehemu Aziza, Mawazo Halid Magumba (32) hali yake ikitajwa kuwa ni mbaya kutokana kupigwa.

" Katika tukio la hivi karibuni polisi wamewapiga na kuwatesa viongozi wetu na wamemuuwa kiongozi wetu mmoja bi Aziza Kibou ambae alikuwa Katibu wa tawi wa ngome ya wanawake. Na Mawazo Halid Magumba katibu wa ngome ya vijana wa tawi hilo ambae ni mume wa marehemu hali yake ni mbaya," alisema Mchinjita.

Mwenyekiti huyo aliwataja wanachama wengine ambao alidai wamepigwa na kuumizwa na ambao wanashikiliwa na jeshi la polisi kuwa ni Nassoro Pingili na Salum Manjocho.

Mchinjita alikwenda mbali kwakusema jeshi la polisi linaonesha kutaka kuficha habari hiyo. Kwani hadi juzi lilikuwa halijaeleza kitu gani kimetokea kuhusiana na kifo cha raia huyo. Badala yake liliwataka ndugu wa marehemu wachukue mwili wakazike kabla hata taarifa ya daktari kuhusu za sababu ya kifo cha Aziza kutolewa.

Kamanda wa polisi( RPC) wa mkoa wa Lindi, kamishna msaidizi wa polisi Mtatiro Kitinkwi ambae leo alikutana na kuzungumza na waandishi wa habari kueleza matukio mbalimbali yaliyotokea na hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo alizungumzia na kutolea ufafanuzi mazingira na kifo cha raia na kada huyo wa ACT- Wazalendo.

Kamanda Kitinkwi alisema tukio hilo lilitokea tarehe 19.12.2020 na sio kweli kwamba jeshi hilo lilikuwa na mpango wa kuficha taarifa za tukio hilo. Kwani halikuwa siri, bali yeye alikuwa nje ya kituo cha kazi. Kwahiyo alishapanga kueleza baada ya kufika ofisini. Hata hivyo matukio yaliyotokea ni mengi. Kwahiyo alitaka aeleze yote kama alivyofanya leo.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda Kintinkwi alisema tarehe 19.12.2020 usiku katika kijiji cha Kibutuka, wilaya ya Liwale jeshi la polisi lilifanya msako kuwasaka watuhumiwa waliochoma moto gari. Ndipo walipokwenda nyumbani kwa Mawazo Halid Magumba ambao baada ya kujitambulisha walimtaka afungue mlango na atoke nje. Lakini Mawazo alikataa kufungua mlango na kutoka nje.

" Askari walivunja mlango, ndipo Mawazo alipotoka nje akiwa na panga. Hali iliyosababisha askari wajihami. Hata hivyo Aziza alikuwa nyuma ya Mawazo akijaribu kuwazuia polisi wasimkamate Mawazo," alisema Afande RPC Kitinkwi.

Alisema katika purushani hiyo Aziza alipigwa risasi ambayo ili mjeruhi na kusababisha kifo chake. Ingawa jeshi hilo halikudhamiria kumuuwa yeyote kati ya hao wawili.

RPC Kitinkwi aliweka wazi kwamba jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kujua mazingira ya tukio la kifo cha marehemu Aziza ili kama ikibainika aliuwawa kutokana na uzembe wa aliyemuua itabidi sheria ichukue mkondo wake kwa muuaji. Kwani hakuna aliye juu ya sheria.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad