ADO SHAIBU: Kamati kuu ilikutana jana jijini Dar es Saalam Tarehe 5 Disemba katika hoteli ya Onomo ambayo iko Posta kwa ajili ya kutafakari hali ya kisiasa inayoendelewa nchini kwetu.
Tumetoka katika uchaguzi uliofanyika tarehe 28 ya mwezi Oktoba, uchaguzi ambao ulitawaliwa na uchafuzi mkubwa sana, uchaguzi ambao umepoteza sifa zote za kuitwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika kwa maana ya free, fair and credible election. Ni uchaguzi ambao laiti kama ungekuwa huru na haki, chama chetu cha ACT-Wazalendo kingepata matokeo makubwa sana.
Ni uchaguzi ambao kwa yeyote yule mwenye jicho la kisiasa ni wazi kabisa ACT-Wazalendo ingeshinda Zanzibar, ingepata wabunge wengi sana, ingepata wawakilishi wengi sana vivyohivyo kwa madiwani kwa sababu chama hiki kilijiandaa kushika dola.
Kamati kuu ilitafakari hali yote hii na kutafakari hatua za kuchukua na hapa nitawasomea azimio lenyewe kwa ajili ya unyeti wake nitalisoma kama lilivyoandaliwa.
Katika mjadala wa kina uliojikita katika maoni yaliyotolewa na wanachama, kamati kuu imezingatia kwamba
Mosi, historia ya kisiasa ya Zanzibar kila uchaguzi tangu uhuru na hata baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi, imekuwa ikigubikwa na hali iliyojaa majeraha, uhasama mkubwa wa kisiasa, watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa, kudhalilishwa kijinsia na mali kuharibiwa. Hali hii imejirudia tena katika uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo watu 17 wamefariki kutokana na matukio mbalimbali ya kwenye uchaguzi ikiwemo watu kupigwa risasi, vipigo na mashambulizi ya kimwili na watu 302 kujeruhiwa na wengine kudhalilishwa kijinsia na mali zao zikiharibiwa na kuibiwa.
Ado Shaibu: Kamati kuu ya chama chetu imeazimia kwamba, wawakilishi wachache kwa maana ya madiwani, wajumbe wa baraza la wawakilishi na wabunge ambao wametangazwa kushinda waruhusiwe kushiriki kwenye vyombo vyao vya uwakilishi ili waendeleze mapambano kwenye vyombo hivyo.