MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi, imemhukumu mfanyabiashara maarufu nchini, Ayubu Kiboko na mkewe Pilly Mohamed kwenda jela miaka 20 kila mmoja kwa makosa ya uhujumu uchumi na kukamatwa na madawa ya kulevya.
Hukumu hiyi imetolewa leo Ijumaa, Desemba 18, 2020 na Jaji wa Mahakama hiyo, Lilian Mashaka ambapo katika Kesi ya msingi namba 29/2018, Kiboko na mkewe wamekutwa na hatia na kukamatwa na madawa ya kulevya na kujihusisha na biashara haramu ya madawa hayo.
Walikamatwa Mei 23, 2018 eneo la Tegeta-Nyuki wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya aina ya heroine zenye uzito wa gramu 251.25 kinyume na sheria.
Mahakama hiyo imesema kuwa, baadhi ya nyaraka na mali ambazo walikutwa nazo washtakiwa hao ambazo hazihusiani na madawa ya kulevya watarudishiwa lakini madawa waliyokamatwa nayo yataharibiwa na serikali kwa kuteketezwa kwa moto.