Changamoto ya Kwanza kwa KOCHA Lwandamina na Azam FC


Kocha mpya wa kikosi cha Azam, George Lwandamina anataraji kuanza rasmi kibarua cha kukinoa kikosi hicho kwa mara ya kwanza leo, watakapowakaribisha 'Wauaji wa Kusini' klabu ya Namungo ya mkoani Lindi kwenye muendelezo wa mchezo wa ligi ya VPL.


Tokea ajiunge rasmi na wanalambalamba hao mapema mwezi huu, Lwandamina hakufanikiwa kusimama kwenye benchi la ufundi kwenye michezo ya miwili iliyopita ya VPL dhidi ya Biashara United na Gwambina FC, kwasababu vibali vyake vya kufanyia kazi nchini havikukamilika.


Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Azam, Abdulkarim Amin 'Popat' amesema, kwasasa vibali vya kufanyia kazi vya kocha huyo vimekamilika na atawaongoza kwa mara ya kwanza na kuwaondoa shaka mashabiki wa Azam kwa kuondoka na alama 3 muhimu kwenye dimba la Chamazi hii leo saa 1:00 usiku.


Kocha Lwandamina ana kibarua kizito cha kuhakikisha Azam FC inapata matokeo na kurudi kwenye njia zake za ushindi, baada ya kuboronga kwenye michezo 7 kwa kutoa sare 3 vipigo 3 na kushinda mchezo 1 na kuporomoka kutoka kileleni hadi kushika nafasi ya 3 kwa kuwa na alama 27.


Kwa Upande wa mgeni wa mchezo huo klabu ya Namungo, mshambuliaji wa klabu hiyo Stephen Sey amesema, "Utakuwa mchezo mgumu ila tunahitaji pointi tatu muhimu kwa kuwa maandalizi yamekwenda vizuri nasi tumejipanga ''.


''Wapinzani wetu tunawaheshimu kwa kuwa ni timu imara na inafanya vizuri hilo lipo wazi ila tutapambana kupata matokeo'', ameongeza Stephen Sey.


Namungo FC ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa VPL mpaka hivi sasa, baada ya michezo 12 na kujizolea alama 16.


Mchezo mwingine wa Ligi Kuu utakaopigwa leo ni kati ya Ihefu FC dhidi ya Kagera Sugar saa 10:00 jioni, kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad