KATIKA majina ya mawaziri waliounda Baraza la Mawaziri lililoteuliwa na Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’, wiki iliyopita, jina la Dorothy Gwajima ni jina lililosababisha gumzo kwa Watanzania wengi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto.
Dk Gwajima amerithi nafasi ya Ummy Mwalimu ambaye katika baraza hilo jipya ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Ummy Mwalimu ambaye amehudumu kwenye wizara hiyo ya afya tangu mwaka 2017, yamkini utendaji wake hasa katika kipindi cha mwaka huu ambao Dunia ilikumbwa na janga la Corona, ndiyo uliowaamisha wengi kuwa atarejeshwa katika wizara hiyo.
Hata hivyo, wengi hawakumfikiria Dk Gwajima ambaye alionekana kuwa injini ya wizara mbili, yaani wizara ya afya pamoja na Wizara ya Tamisemi-(Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).
NINI KILICHOMBEBA?
Yamkini baadhi ya Watanzania hawamfahamu vema mwanamama huyu ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu.
Kwa mujibu wa baadhi ya watumishi waliofanya naye kazi, wameweka wazi kuwa hakuna kingine zaidi ya utendaji wake uliosheheni, weledi, uadilifu na ufuatiliaji.
Kauli za watumishi hao waliozungumza na Ijumaa bila kutaja majina yao, zinaendana na matokeo ya utendaji wa kiongozi huyo katika nafasi alizopitia.
Tukiachana na nafasi ndogo zilizoanza kumjenga kitaaluma na kiuongozi, awali Dk Gwajima alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hadi kufikia Januari mwaka jana ambapo ndipo Rais Magufuli alimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya).
Nafasi hizo mbili zinadhihirisha ni namna gani mwanamama huyo alivyomudu kuzihudumia wizara hizi mbili ambazo zimejichotea sifa kedekede katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Magufuli.
MFICHUA MAOVU
Alipoingia madarakani baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu mwaka jana, Dk Gwajima alianza kula sahani moja na wabadhirifu wa dawa.
Hili ni jambo ambalo alilikazia kila mahali katika ziara zake ambapo aliapa kuwa moto dhidi ya wabadhirifu wa dawa aliouwasha katika zoezi la ufuatiliaji hautazimika wala kupoa.
“Niwaombe wanachi kuwa mstari wa mbele kufichua wale wote mtakaowabaini wanahujumu suala la dawa kwani vita hiyo siyo ya mtu mmoja mmoja wala Serikali peke yake, bali ni ya jamii nzima.
“Wapo watu wanaotambua nani ni adui wao katika vita hivi ndiyo maana niliona kwenye mitandao ya kijamii watu wakinipa pole na kunipongeza, lakini nasema lazima tutembee na wananchi katika hili.”
Hiyo ni kauli ya kiongozi huyo wakati akizungumza na Makatibu Tawala wa Mikoa, wataalamu Wafamasia kutoka mikoa 13 na wadau wa maendeleo, waliokutana Oktoba mwaka jana jijini Dodoma katika kikao kazi cha tathmini ya mbinu mpya ya kuimarisha takwimu za bidhaa za afya.
Matokeo ya kazi na ufuatiliaji huu wa Dk Gwajima yameendana na matokeo yake kwa sababu Mei, mwaka jana, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD), Laurean Bwanakunu.
Aidha, Juni mwaka jana Bwanakunu na Byekwaso Tabura ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matano likiwemo la kuisababishia MSD hiyo hasara ya zaidi ya Sh.Bil 3.8.
Matokeo ya kauli ya Dk Gwajima hayakutafuna kambale pekee kwani hata dagaa walinaswa kwa sababu Juni hiyohiyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, iliwanasa wafanyakazi 30 wa MSD mkoani humo, kwa tuhuma za ubadhirifu wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 254.
MAFANIKIO YALIVYOMBEBA
Ni dhahiri kuwa mafanikio yaliyopo katika sekta ya afya hayawezi kutajwa bila kuwepo kwa jina la mwanamama huyu ambaye ameisaidia sekta ya afya nchini kuleta mapinduzi ya kipekee hasa baada ya Rais Magufuli kuelekeza bajeti kubwa katika wizara ya afya kuliko wizara nyingine zozote.
Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 12 la Novemba, mwaka huu, Rais Magufuli alisema sekta ya afya imepata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 (zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3.
“Vilevile tumepunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka wastani wa vifo 11,000 kwa mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa 3,000 hivi sasa na halikadhalika rufaa za kupeleka wagonjwa nje zimepungua kwa asilimia 90 baada ya kuimarisha huduma za kibingwa,” alisema.
WATALAAM WAMPA HEKO
Baadhi ya wataalam wa sekta ya afya waliozungumza na Gazeti la IJUMAA, akiwamo Dk Vincent Mashinji ambaye mbali na kuwa mwanasiasa pia ni msomi katika sekta afya, alisema kwa mtazamo wa nje wa harakaharaka inaonekana angefaa zaidi kwenye nafasi ya Katibu Mkuu.
“Kwa sababu Dk Gwajima ni mtendaji kuliko mwanasiasa na nafasi uwaziri aliyopewa ni ya kisiasa.
“Lakini falsafa ya Rais ni kubadilisha mfumo wa utendaji, badala ya watu kuwa na blaahblaah, sasa wanaelekezwa kuwa watendaji zaidi.
“Kwa hiyo dhana nzima ni kwamba Serikali inakuwa ya utendaji kuliko maneno ya porojo. Hii imeendana kabisa na Dk Gwajima ambaye pia anaendana na falsafa nzima ya Rais,” alisema.
Dk Mashinji aliongeza kuwa Dk Gwajima ni kiongozi ambaye hana makandokando ya rushwa, ni mtulivu na mwerevu hivyo kama wafanyakazi wa wizara ya afya watakuwa makini na kumpa ushirikiano, ataisogeza mbali wizara hiyo.
DK GWAJIMA NI NANI?
Dk Gwajima amebobea katika masuala ya afya ambapo mwaka 2009 alihitimu shahada ya uzamili katika masuala ya afya ya umma (MPH) katika Chuo Kikuu cha Royal Tropical Institute kutoka Uholanzi. Mwaka 2001 alihitimu Shahada ya kwanza ya masuala ya dawa kutoka Chuo cha Nizhniy Novgorod Medical Academy-Urusi.
Dk Gwajima (49) ambaye ni mzaliwa wa Iramba mkoani Singida, amehudumu katika fani ya udakari katika ngazi mbalimbali kwa kuanzia katika Hospitali ya Wilaya Bagamoyo, Mganga Mkuu wa Wilaya Iramba, Mganga Mkuu wa Mkoa Singida na nafasi nyingine kabla ya kupanda hadi kuwa Naibu Katibu Mkuu kisha Waziri wa Afya.
IMEANDALIWA GABRIEL MUSHI