Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amemteua naibu katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Nassor Ahmed Mazrui na mwanasheria mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Dk Mwinyi amefanya uteuzi huo Jumatatu Desemba 7, 2020 ikiwa imepita siku moja baada ya kumteua mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa leo na katibu mkuu kiongozi, Dk Abdulhamid Mzee inaeleza kuwa uteuzi huo ni kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu namba 66 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Dk Mwinyi amefanya teuzi hizo baada ya ACT-Wazalendo kuridhia kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).