Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema kuwa leo Disemba 2, 2020, dirisha la rufaa limefunguliwa rasmi kwa waombaji ambao hawajapangiwa mikopo na wale ambao hawajaridhika na viwango walivyopangiwa, waambatanishe nyaraka za ziada ili kuthibitisha uhitaji wao.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru, wakati akitangaza orodha ya awamu ya tatu yenye jumla ya wanafunzi wapya 3,544, waliopangiwa mikopo kwa mara ya kwanza yenye thamani ya shilingi bilioni 11.04.
"HESLB inatoa wito kwa wanafunzi ambao bado hawajapangiwa mikopo na ni wahitaji, kutumia muda wa siku saba (07) za rufaa kuwasilisha nyaraka sahihi ili hatimaye wapangiwe mikopo ya kuwawezesha kulipia gharama za masomo", amesema Mkurugenzi wa HESLB.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika kipindi cha rufaa, wanafunzi watahitajika kutembelea mfumo wa olas.heslb.go.tz, kufuata maelekezo na kuwasilisha rufaa zao kutoka popote walipo na bila malipo yoyote.