Ligi kuu soka Tanzania bara raundi ya 16 itaanza kutimua vumbi leo kwa michezo 4, ambapo michezo hiyo itachezwa katika miji 4 tofauti, mkoani Shinyanga, Mara, Kagera na Jijini Dar es salaam.
Mchezo wa mapema hii leo utachezwa mkoani Shinyanga Saa 8:00 Mchana, katika dimba la Mwadui Complex ambapo Mwadui watakuwa wenyeji wa Polisi Tanzania ya Moshi, wenyeji wa mchezo huo Mwadui ndio wanaoburuza mkia kwenye msimamo wa ligi kuu wakiwa na alama 10 kwenye michezo 15, wakati Polisi wapo nafasi ya 6 wakiwa na alama 21.
Saa 10:00 jioni itachezwa michezo miwili mkoani Mara katika dimba la Karume Biashara United watakipiga dhidi ya Mbeya City, Mbeya City hawajawahi kuifunga Biashara kwenye michezo 4 ya ligi kuu, katika michezo hiyo Biashara wameshinda mara 3 na sare 1, wenyeji Biashara wapo nafasi ya 8 wakiwa na alama 20 wakati Mbeya City wanaalama 12 wakiwa nafasi ya 16.
Mchezo mwingine wa Saa 10 Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, msimu uliopita katika dimba hilo Kagera waliibuka na ushindi wa bao 1-0, na timu hizi zinaingia kwenye mchezo wa jioni ya leo zikiwa zinalingana alama zote zina alama 18, katika idadi sawa ya michezo 15, huku Kagera Sugar wakiwa juu ya Costal kwa faifa ya mabao ya kufunga na kufungwa Kagera wapo nafasi ya 11, Coastal wapo nafasi ya 12.
Mchezo wa mwisho hii leo utachezwa Jijini Dar es salaam saa 1 usiku uwanja wa Azam Complex, ambapo Azam FC watakuwa wenyeji wa Ruvu shooting, katika msimamo wa ligi timu hizi zinatofautiana alama 4, Azam wapo juu ya Ruvu shooting wakiwa na alama 28 katika nafasi ya 3, wakati Ruvu shooting wapo nafasi ya 4 wakiwa na alama 24.
Na katika michezo 5 ya mwisho timu hizi kukutana Azam kashinda mara 2 kafungwa mara 1 na wametoka sare 2, ukiwemo ushindi wa mabao 2-1 katika dimba la Azam Complex msimu uliopita