KIUNGO wa Simba Jonas Mkude juzi alitangazwa kuondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo kutokana na utovu wa nidhamu.
Mkude amekuwa akikumbana na rungu la utovu wa nidhamu mara kwa mara kwenye kikosi cha Simba na sasa uongozi wa timu hiyo umeamua kumsimamisha.
Simba hawajaweka wazi sababu za kumuondoa kiungo huyo, ingawa chanzo cha ndani kinasema kuwa amefanya mfululizo wa makosa, huku ikidaiwa kuwa anafanya makusudi.
Chanzo hicho kimesema kuwa awali ilikuwa inaelezwa kuwa chanzo cha utovu huo wa nidhamu ni utumiaji wa kileo, lakini siyo kweli bali mara zote amekuwa mzima kabisa wakati anafanya matukio hayo.
“Kwanza amekuwa akichelewa mazoezini makusudi, lakini wakati mwingine amekuwa ananuna tu bila sababu zozote.“Kwa wiki mbili nafikiri amechelewa mara tatu na hana majibu sahihi kila anapoulizwa, sasa hata kama mtu unataka kuondoka au una ishu yako basi ipeleke kwa uongozi,” kiliseme chanzo chetu.
Inaelezwa kuwa kiungo huyo hatakuwepo kwenye mchezo dhidi ya Ihefu leo, lakini atakuwa ameshakutana na kamati ya nidhamu ya Simba kabla ya kuvaana na Platnum, Januari 6 na anaweza kurejea uwanjani.
NA Mwandishi Wetu, Dar es Salaam