Jaji Mkuu Atoa Tamko kwa Mawakili wa Kujitegemea




JAJI Mkuu  Prof. Ibrahim Hamis Juma, amewaasa mawakili wapya wa kujitegemea kuwawakilisha vyema wananchi wanaosimamia kesi zao mahakamani kwa kufuata sheria na kanuni stahiki za uwakili na kuziishi kanuni za kimaadili, nidhamu na tabia njema za Mawakili.

 

Akitoa hotuba yake mara baada ya kuwakubali na kuwapokea mawakili hao mapema leo Desemba 21, 2020 katika Viwanja vya Karimjee-Dar es-Salaam, alisema kuwa kuna baadhi ya mawakili wamekuwa si waaminifu.

 

“Sote tunafahamu kuwa katika kazi zenu za uwakili mtawajibika kwa wateja wenu watakaowapa ajira. Lakini kumbukeni kuwa wajibu mnaotakiwa kuupa uzito wa juu zaidi ni wajibu wenu kwa katiba, kwa sheria za nchi na kwa mahakama mkiwa maafisa wa mahakama,” alisema.

 

Aliongeza kwa kuwasisitiza mawakili hao kuwa ni wajibu wao kuhakikisha kuwa hawawaingizi wateja wao/wananchi katika uvunjifu wa sheria pamoja na kanuni za kimaadili, nidhamu na tabia njema za mawakili (the advocates (professional conduct and ettiquette) regulations, 2018 gn no. 118 of 2018) ambazo tayari zinatumika kuwaongoza katika kazi za uwakili.

 

“Bado ipo mifano inayoashiria kuwa wapo mawakili wachache ambao bado hawaziishi kanuni tajwa za mawakili, kila siku katika mitandao ya kijamii, hasa ya TWITTER, tumeona wakitumia lugha zisizofaa (wengine waziwazi, wengine kwa majina ya kubuni). Wapo mawakili ambao wamejipambanua kwa kupotosha tafsiri ya maamuzi ya mahakama na kuivuta mahakama katika malumbano ya kisiasa,” alifafanua.

 

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa aliwataka mawakili hao kuwa sehemu kubwa ya kuisaidia mahakama kufikia maamuzi ya haki.

 

“Niwakumbushe tu kwamba sasa mtakuwa maafisa wa mahakama chini ya Sheria ya Mawakili, Sura ya 341. Hivyo mtakuwa na wajibu kwa mahakama na kuhakikisha mnaisaidia mahakama kufikia kwenye maamuzi ya haki na yanayotolewa kwa wakati,” alisema.

 

Naye Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Dkt. Rugemeleza Nshala aliwataka mawakili hapo kujiweka sawa katika matumizi ya lugha, Kiswahili na Kiingereza fasaha kwani lugha ni jambo muhimu katika kazi ya uwakili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad