Jangwani kupatiwa ufumbuzi kabla ya masika kuanza

 


Serikali kupitia Mfuko wa Barabara (Road fund), imesema ipo tayari kupitisha kiasi cha shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kumlipa mkandarasi atakaepatikana ili kuboresha miundombinu ya eneo la Jangwani, jijini Dar es Salaam, mara baada ya uhakiki wa makisio hayo kukamilika na kujiridhisha.

 

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya mfuko huo, Mwenyekiti wa Bodi, Joseph Haule, amesema kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha inatatua changamoto hiyo haraka kabla ya mvua za masika kuanza.


"Bodi imeona tatizo hili na tumeliona kama suala la dharura, ndiyo maana tumekuja hapa kujionea hali halisi ili kutafuta njia sahihi ya kutatua tatizo hili ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu", amesema Mwenyekiti wa Bodi.


Aidha Haule amefafanua kuwa kweli tatizo ni kubwa, mfereji una kina kifupi na makalavati mawili makubwa yaliyopo hapo yameziba kabisa na kuongeza kuwa nia ya Bodi ni kuona wananchi na wasafirishaji wanatumia miundombinu hiyo wakati wote wa mvua na kiangazi.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, amesema kuwa serikali kupitia Wizara yake imeandaa mkakati wa muda mrefu kuhusu miundombinu hiyo, ambapo amesema kwa sasa wataalamu wanafanya usanifu wa kina kwa ajili ya kuja na suluhisho la kudumu ikiwemo ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 300.


Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, wametembelea eneo la Jangwani kujionea hali halisi ya miundombinu katika eneo hilo ambayo imekuwa ikiathiriwa na mvua na kusababisha kufunga mawasiliano ya watumiaji wa barabara ya Morogoro hususani eneo hilo kila mwaka.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad