MBUNGE wa Jimbo la Bumbuli Mkoani Tanga, January Makamba amewataka madiwani na viongozi wote waliiochaguliwa kuongoza halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli kujitoa na kuyachukulia mapambano ya maendeleo wa wananchi kama jihad.
Akizungumza katika katika kikao cha Kwanza cha Madiwani kilichofanyika Bumbuli alisema kuwa bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wananchi wa Halmashauri hiyo licha maendeleo yaliyofanyika katika kipindi cha miaka saba tangu ianzishwe.
Mbunge huyo alisema kuwa Halmashauri hiyo bado ni changa kama taasisi na akasisitiza kuwa mahali ambapo kuna changamoto kubwa za maendeleo zinahitaji moyo mkubwa wa kujitoa.
Makamba alieleza kuwa sababu kubwa ya kuanzishwa kwa Halmashauri ilikuwa ilionekana iko pembeni kimaendeleo hivyo kuhitaji uwepo wa taasisi itakayokuwa karibu na wananchi kukabiliana na changamoto nyingi za maendeleo.
“Hata mimi nilipoamua kuomba ridhaa wa wananchi kuwa mbunge nilifanya hivyo kwa sababu nilikuwa nataka nitoe mchango wangu katika maendeleo ya Bumbuli,” alisema Makamba.
Alieleza kwamba mpaka sasa bado changamoto zipo na kueleza kuwa anaamini kuwa wote waliochaguliwa walisukumwa na moyo huo huo.
Mbunge huyo alisema kuwa hakuna sababu ya kuona aibu kwa ajili hali halisi ya mambo ilivyo katika halmashauri hiyo.
“ Yaani Utaona mtu anapiga picha basi limekwama kisha anarusha katika mitandao akidhani ni aibu jamani Hiyo ni hali halisi, ndiyo maana tunatoa hata pesa zetu mfukoni kutengeneza miundo mbinu hata pesa ya serikali inapochelewa,” alieleza.
Aliahidi kushirikiana na wataalamu wa halmashauri hiyo akisema kuwa wanategemea sana wekedi wao na uadilifu wao katika kuleta maendeleo katika halmashauro hiyo.
Hata hivyo, aliwataka wataalamu nao waelewe shinikizo walilonalo viongozi wa kuchaguliwa kutokana na matarajio makubwa ya wananchi hivyo wanapokosoa au wanaposhinikiza ni kwa nia njema.
Alisisistiza kuwa pale watapoona mmoja wa wataalamu anachelewesha watasema bila kuogopa.
“Tunafanya kwa nia njema na kwa uwazi kwani Ubaya ni kumuazimia mtu kwa fitina , uongo, majungu na taarufa zisizo kamili,” alisema na kuwataka madiwani kutokufanya hivyo kwa sababu inaleta vurugu isiyokuwa na sababu.
Alisema kuwa kipindi hiki watasukuma maendeleo kwa nguvu kubwa ili kutengeneza rekodi kubwa na nzuri hata kama hawataweza kumaliza shida zaote miaka mitano ikiisha.
“Tupambane katika maendeleo kama jihad ili tuje kuonyesha kuwa pale kuna zahanati, darasa, shule, barabara au kuna maji kutokana na kazi tulizofanya,” alisema Makamba ambaye ni Mbunge wa Bumbuli Mkoani Tanga
Akizungumza katika kikaohcho ambacho kilimchagua Diwani wa Kata ya Soni, Amiri Shehiza kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Judica Omari alisisitiza juu ya umuhimu wa viongozi hao kuhakikisha sheria za serikali na kanuni zinatekelezwa na wananchi wanazielewa a kuzitimiza.