Je Museveni Anatumia Mbinu Gani Kusaka Kura za Walalahoi?

 


Kinachovutia hasa sio kipaji cha mchoraji namna alivyoipatia sura hiyo. Bali ni sentensi ya maneno manne pembeni ya mchoro, yakisomeka, "M7 Man of Ghetto".



Ni dhahiri mchoro huo unaakisi juhudi za mkongwe huyo wa umri na katika siasa, kutafuta ushawishi na uungwaji mkono katika tabaka la vijana na raia wa kipato cha chini.




Ukuta wa jengo hilo ni ofisi ya vijana wa chama tawala National Resistance Movement (NRM). Mchoro huo haukuwepo awali, ulichorwa miezi mitatu baada ya Robert Kyagulanyi Ssentamu ama Bob Wine, kutangaza Julai 2019 kuwa atawania kiti cha Urais katika uchaguzi wa Januari 14, 2021.




Ukizama ndani katika ofisi, moja ya shughuli inayofanyika hapo, ni kuwawezesha kiuchumi vijana wanaoishi na kufanya kazi katika eneo la Kibuye na Katwe. Shughuli ambayo haikufanyika kabla ya joto la uchaguzi.




Juhudi za Rais Museveni kuhakikisha anazipata kura za vijana na kukubalika katika tabaka la walalahoi, haziishi tu katika mchoro. Pia, amewatumia wana muziki kama Bebe Cool, Catherine Kusasira, Jose Chameleone, Butcherman, Eddy Kenzo na Full Figurez ili kutafuta mvuto kuelekea uchaguzi mkuu.




Wadadisi wa mambo wanaamini mbinu ya kuwatumia wasanii haina lengo la kuwavuta tu vijana, pia ni kumgonganisha Bob Wine ambaye kabla ya siasa alikuwa msanii na wasanii wengine wakubwa katika taifa hilo.




Tangu pirikapirika za uchaguzi zianze nchini humo, Rais huyo ameonekana kuwa hai zaidi katika mitandao ya kijamii. Yumkini ni mbinu ya kushindana na Bob Wine ambaye anaitumia vyema mitandao hiyo kupambana na kukosoa utawala wake.




Rais wa Ghetto vs Mtu wa Ghetto


Hadi sasa picha kubwa ya uchaguzi wa Uganda inaonesha vita vikubwa vya kuwania kiti cha Urais ni kati ya Museveni ajiitae Mtu wa Ghetto na Bob Wine, kwa lakabu ya Rais wa Ghetto. Wawili hao ndio wanaovuma zaidi kuliko wagombea wengine.




Licha ya Museveni kuwa mmoja wa viongozi waliokaa muda mrefu madarakani katika bara la Afrika, akiwa Rais kwa miaka 34. Bado muasi huyo wa zamani anatafuta tena kuendelea kubaki katika kiti hicho.




Lakini mwanasiasa kijana mwenye umri wa miaka 38 na Mbunge wa eneo bunge la Kaunti ya Kyadondo, Mashariki, Robert Kyagulanyi, ana mpango mbadala dhidi ya Museveni. Kupitia chama cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa-UNP, mpango wake ni kumtoa Ikulu kwa kura katika uchaguzi wa Januari 2021.




Kuna ukosefu mkubwa wa ajira miongoni mwa vijana na kundi kubwa la raia wanaoishi katika umasikini. Museveni anajaribu kubuni mbinu ili kuwepo daraja kati yake na wapiga kura hao ambao wengi wao hawamtaki tena.




Bob Wine na ujumbe wake wa kukemea ufisadi, vurugu na matumizi mabaya ya madaraka, amekivuta kizazi cha vijana na watu wa hali chini, hadi kuwa mwanasiasa pendwa kwa makundi hayo.




Sasa ni rahisi kumshinda Museveni?


Mwishoni mwa mwaka 1986, Museveni alifanya mkutano na waandishi wa habari katika mji wa Bonn nchini Ujerumani. Alikuwa na ziara katika mataifa ya Ulaya baada ya ushindi wake wa vita vya msituni.




Mmoja wa waandishi wa habari kutokea Deutsche Welle alimuuliza; mna ajenda ya kubakia muda gani madarakani?




"Hatukupigania mabadiliko ili tutamalaki kwenye uongozi. Hatukuja kukaa, sisi ni tofauti na waliotangulia na tulio waondoa".




Miaka 19 baada ya kauli hiyo. Agosti 2005 Bunge la Uganda liliondosha ukomo wa mihula ya Urais. Huo ukawa mlango wa kwanza kwa Museveni kuendelea kulitawala taifa hilo la Mashariki mwa Afrika.




Ilipofika Julai, 2018, mahakama ya kikatiba nchini humo ilihalalisha sheria iliyoondoa ukomo wa umri kwa Rais. Sheria ya awali ilimzuia mtu yeyote aliye na umri wa kuazia miaka 75 na kuendelea kugombea urais.




Ulikuwa ni mlango wa pili wa kumbakisha Museveni Ikulu. Wapinzani wake kisiasa wanamlaumu kwa mabadiliko hayo, wakiamini kuna mkono wa Museveni na chama chake.




Museveni mwenye umri wa miaka 76 bado ana nguvu kubwa katika siasa za Uganda. Amejenga ngome imara akiwa na uhakika wa uungwaji mkono kutoka vikosi vya usalama vya nchi hiyo.




Tatizo la Uganda linafanana na tatizo sugu lililopo katika baadhi ya mataifa ya Afrika; kukosekana taasisi za kuaminika katika kusimamia uchaguzi na kuwepo kwa vikosi vya usalama vinavyosimama upande wa chama tawala na kukandamiza upinzani.




Katika mazingira hayo, ugumu unazuka wa kufanyika uchaguzi huru na haki. Kwa maneno mengine, nguvu za vyama vya upinzani kutoka kwa vijana na wafuasi wao kwa ujumla, zinaweza kutoka patupu kwa sababu tu nchi ina taasisi zenye walakini katika kusimamia uchaguzi.




Hivyo Bob Wine na wafuasi wake, hawapambani tu kumtoa Museveni madarakani. Pia, wanapambana na ile mifumo inayoweza kumrudisha Rais huyo madarakani hata ikiwa idadi ya kura hazitomtosha kuendelea kubaki kuwa Rais.




Mwaka 2001 Rais Museveni alijifananisha na kotapini kwenye pedali ya baiskeli, ambayo huingizwa kwa nyundo, na kutolewa kwa nyundo. Huu ulikuwa ni ujumbe kwa wapinzani wake kwamba wasidhani ni rahisi kumtoa katika kiti.




Ingawa kuna mashaka kuhusu uwezo wa Uganda kuendesha uchaguzi huru na haki na utayari wa Museveni kuondoka madarakani endapo atashindwa. Kwa upande mwingine, nguvu ya Bob Wine na wafuasi wake inabaki kuwa kitisho kikubwa kwa utawala huo wa miongo mitatu, licha ya mashaka hayo.


 

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Upinzani huwa Haukandamizwi kama usemavyo, Upinzani huwa hauna mvuto naUshawishi kwa kukosa Sera za kuuza kwa Wananchi,, hatima yake ni Kupandikizwa kwa watu ambao watatumikia mabwana walio wapandikiza na mwisho wa siku kitengo cha wafu (joji bushy na Magaleti Tacha -IDU) Kuwapa hogela Mlijaribu ila bahati mbaya Wananchi hawakuwaelewa.

    Sasa, kama kwa Mzee Museveni, Kweli kuna mpinzani wa kuweza kushika nchi..?? Tuseme ukweli. Labda watu wamechoka lakini nani kama ni mbadala..HUKUNA..!! Mcheza Disko kama Mtowe..??

    Are you serious ..!!!

    Museveni Jembe, Anatuletea bomba toka Hoima mpaka Tanga.
    Mcheza disko atakuwa Mlafi na kuboresha studio ya music production kama Billicanas ndiyo ilitokea kwetu na kusepea
    Ubelijiji,Tuwaombee Waganda Amani na Utulivu na Wampee kura nyingi za Kishindo Mzee Yoweri Kaguta, Museveni Oyeee!!!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad