KWA mara ya kwanza Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck anatarajiwa kumtumia kiungo mkabaji Thaddeo Lwanga kwenye mchezo wa leo dhidi ya FC Platinum ya nchini Zimbabwe.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo Jumatano katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe uliopo kwenye Mji ya Harare.
Lwanga aliyepo kwenye msafara wa timu hiyo uliokwenda Zimbabwe, alisajiliwa na Simba katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa Desemba 16, mwaka huu katika kuiboresha safu ya kiungo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa timu hiyo, Abbas Ally, alisema kuwa wamefanikiwa kupata leseni ya kiungo huyo itakayomuwezesha kucheza mchezo wa leo huko Platinum.
Abbas alisema kuwa wamefanikiwa kupata kibali hicho baada ya jitihada za kutosha zilizofanywa na viongozi wa timu hiyo waliosafiri na msafara huo ulioongozwa na Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Barbara Gonzalez.
“Uongozi umefanikiwa kupata kibali cha Lwanga ni baada ya kufanya jitihada za kutosha ili kuhakikisha Caf wanatoa kibali kitakachomruhusu kucheza mchezo huo.“
Hadi kufikia jana hatukuwa na uhakika wa kumtumia Lwanga lakini mara baada ya kupata kibali sasa tumepata uhakika wa kumtumia, lililobakia ni jukumu la kocha kuamua kumtumia au kutomtumia,” alisema Abbas.
Stori: Wilbert Molandi,Dar es Salaam