Dar es Salaam. Desemba 23, siku mbili kabla ya Sikukuu ya Krismasi, wanaume jijini hapa walialikwa katika sherehe ya kuburudika na wanawake wawatakao lakini Jeshi la Polisi limeifuta sherehe hiyo na kuwatia mbaroni waandaaji wake.
Ni sherehe ya ufuska iliyopangwa kufanyika eneo la Mbezi Beach jijini hapa, ambayo mhudhuriaji alitakiwa kununua kadi itakayomuwezesha kuingia katika nyumba maalum na humo angekutana na wanawake wa kustarehe nao.
Kwa utaratibu uliowekwa, kulikuwa na kadi ya Sh150,000 ambayo mwanaume angepata mwanamke mmoja na ya Sh300,000 inayompa fursa ya kujipatia wanawake wawili wa kufanya nao uzinzi.
Maandalizi ya sherehe hiyo yalipangwa na kutangazwa katika mitandao ya kijamii lakini Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni lilibaini jambo hilo na kuwakamata watano, akiwamo mwandaaji wa sherehe hiyo.
Video mbalimbali zilizosambaa mtandaoni zina sauti ya mtu anayefafanua kuhusu upatikanaji wa kadi hizo, akisisitiza kuwa siku hiyo mambo yatakuwa mazuri na kuwataka wateja kuwahi kuzinunua.
Wakati sauti hiyo ya kike ikisikika kueleza hayo, katika video ilikuwamo namba ya simu kwa watakaotaka kushiriki huduma hiyo ambayo hata gazeti hili lilipojaribu kuipiga haikupatikana na wakati likiendelea na uchunguzi, polisi walibainisha kuwakamata watu hao huku jeshi likiendelea kuusaka mtandao mzima unaojihusisha na ufuska huo.
Akizungumza na gazeti hili, kamanda wa polisi, Ramadhani Kingai alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi usiku na bado wanaendelea kuwatafuta wengine waliosambaza video hizo.
“Tumemkamata mwandaaji wa shughuli hiyo, tunaye pamoja na wengine wanne waliosambaza video hizo. Bado tunawatafuta wengine walioisambaza,” alisema.
Alisema jeshi limeingilia kati sherehe hiyo kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume na utamaduni wa Watanzania na ni kinyume na sheria za nchi.
“Ni kosa kusambaza video inayohamasisha ngono, kusambaza taarifa ile pia ni kinyume na sheria ya makosa ya mtandaoni hivyo tunaendelea na uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema kamanda Kingai.
Mbali na kupata mwanamke wa kuburudika naye, mwanaume ambaye angehudhuria sherehe hiyo angepewa chumba, kuogelea na kupata huduma nyingine.
“Hizi ndio tiketi zetu... hii ni ya Sh300,000 unapata wanawake wawili wa kufanya nao mapenzi na ya Sh100,000 unapata mwanamke mmoja wa kufanya naye mapenzi. Kwenye hii tiketi utapata chumba, utaogelea na shoo yangu ya (anaitaja), wote mnakaribishwa Mbezi Beach private house,” anaeleza mwanamke huyo kwenye video inayosambaa mtandaoni.
Baadhi ya waliotoa maoni kuhusu video hiyo walitaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao na kwa uwazi ili iwe fundisho kwa wengine.
“Sisi Watanzania haya mambo si utamaduni wetu, sisi ni wastaarabu sana, tusipende kuiga vitu vya nje. Zichukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizi,” alisema Juma Omary mkazi wa Tabata jijini hapa.
Naye Lucy Athumani alisema endapo Jeshi la Polisi lisingechukua hatua dhidi ya wahusika hao, lingeonekana linabariki sherehe hiyo ambayo ni aina mpya ya watu kuuza miili yao.
“Kuwakamata haitoshi inabidi wachukuliwe hatua kali ili wengine wajue kufanya hivyo ni kosa kisheria na hawatakiwi kujaribu,” alisema Lucy.