IMEFAHAMIKA kuwa mshambuliaji tegemeo wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere, amemalizana kwa asilimia tisini na Klabu ya Yanga iliyokuwa inawania saini ya nyota huyo kwa muda mrefu.
Yanga inataka kumsajili Mnyarwanda huyo kwa ajili ya kuiboresha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongozwa na Mghana, Michael Sarpong, Yacouba Songne na Ditram Nchimbi.
Mnyarwanda huyo hivi sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kufanya mazungumzo ya awali na klabu nyingine kutokana na kubakiza miezi sita katika mkataba kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Yanga tayari imempa mkataba wa awali wa miaka miwili mshambuliaji huyo aliyetwaa kiatu cha ufungaji bora kwa misimu miwili mfululizo.
Alijiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya nchini Kenya.Mtoa taarifa huyo alisema kiungo huyo anatarajiwa kujiunga na Yanga msimu ujao mara baada ya mkataba wake kumalizika kuendelea kukipiga Simba aliyojiunga nayo msimu wa 2017/2018.
Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo ataondoka Simba kutokana na kutokuwa na uhusiano mzuri na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji ambaye amekuwa akimkalisha benchi katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
“Yanga imemalizana na Kagere kwa asilimia kubwa, kwani tayari amesaini mkataba wa awali wa miaka miwili ya kuichezea Yanga baada ya kufikia muafaka mzuri na timu hiyo.“Kagere atajiunga na Yanga kwenye msimu ujao baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika ya kuendelea kuichezea Simba na hiyo ni baada ya kuonekana kocha huyo hana mahusiano mazuri.“
Yanga inataka kumsajili Kagere katika kuiimarisha safu ya ushambuliaji ambayo imeonekana kutofunga mabao mengi, hivyo anajiunga na timu hiyo kwa ajili ya kusaidiana na akina Sarpong,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’, hivi karibuni alisema kuwa hawatakubali kumuachia mchezaji yeyote muhimu na tegemeo katika timu hiyo kwa kuhofia kukivunja kikosi chao akiwemo Luis Miquissone anayewindwa na klabu kadhaa zikiwemo kutoka Ulaya.