Moshi. Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro limetoa tahadhari kwa wananchi wanaoingia mkoani humo kwa ajili ya kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka likiwataka kuzingatia sheria za barabarani ili kuepuka ajali.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 18, 2020 na kamanda wa polisi mkoani humo, Immanuel Lukula katika mkutano wake na waandishi wa habari
Amesema hali ya usalama mpaka sasa mkoani humo ni shwari na kuwataka wageni wanaoingia kutoka mikoa mbalimbali na nchi jirani kutunza hali ya amani na utulivu iliyopo.
"Jeshi la polisi tuna mpango kazi mzuri, hasa kwenye kitengo cha usalama barabarani, niwasihi wana kilimanjaro kuzingatia mambo makuu mawili.”
"Moja kuelekea sikukuu hizi, nawasihi wageni waliokuja na wanaoendelea kuingia mkoani hapa kutokunywa pombe na kuendesha chombo cha moto, Pili kutoendesha mwendo kasi kwani haya yote yanaweza kusababisha ajali,” amesema Lukula.