BAADA ya ushindi wa kibabe wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji Jumamosi iliyopita, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amefunguka kuwa mipango yake ni kuhakikisha anakusanya pointi tatu kwenye mchezo ujao dhidi ya Ihefu, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Ushidi huo wa tano mfululizo kwa Yanga, umeifanya kufikisha pointi 40 baada ya kucheza michezo 16, imeshinda michezo 12 na kutoa sare nne pekee, huku mpaka sasa ikiwa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo tangu kuanza kwa ligi ya msimu huu.
Yanga sasa imebakisha mchezo mmoja pekee kukamilisha ratiba yake ya mzunguko wa kwanza ambapo tofauti na msimu uliopita msimu huu kwenye mzunguko wa kwanza timu zitacheza michezo 17, kwa kuwa timu shiriki ni 18.
Kaze ameliambia Championi Jumatatu, kuwa mipango yao ndani ya mzunguko huu wa kwanza ni kuhakikisha wanamaliza wakiwa kileleni mwa msimamo, jambo ambalo litaongeza nguvu na morali ya wachezaji kufanya vizuri mzunguko wa pili katika malengo yao ya kutwaa ubingwa.
“Nafurahi kuona kikosi changu kina morali kubwa ya kupambana kwenye kila mchezo kwa ajili ya kusaka matokeo, mpaka sasa tunaongoza msimamo na hayo ndiyo malengo yetu.
“Tunataka kuhakikisha tunashinda mchezo wetu dhidi ya Ihefu ili kusalia kileleni mwa msimamo wakati wa kutamatisha mzunguko huu wa kwanza.
“Kwa kufanya hivyo ni wazi tutaongeza ari ya kikosi chetu kuelekea michezo ya raundi ya pili ambayo tunapaswa kufanya vizuri zaidi ili kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema Kaze.
JOEL THOMAS, Dar es Salaam