PWANI: Kifo cha Mwalimu Joyce Ismail (35) wa Shule ya Msingi ya Ruvu-Darajani mkoani Pwani, kimeibua sintofahamu nzito na mshangao kwa wengi.
Mwalimu Joyce anadaiwa kuuawa kinyama kwa kuchinjwa na mumewe ambaye ni Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Daniel Warioba (43) kutoka Kikosi cha 92 TJ mkoani Pwani.
Ilidaiwa kwamba, baada ya kutenda unyama huo, jamaa huyo alifanya jaribio la kujiua kwa kunywa sumu kabla ya kukamatwa kisha kupelekwa Hospitali ya Tumbi kunusuru uhai wake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Wankyo Nyigesa, tukio hilo lilijiri muda wa usiku nyumbani kwa wanandoa hao katika eneo la Janga, Wilaya ya Kipolisi Mlandizi.
Kamanda Wankyo alisema askari huyo anadaiwa kumchinja mke wake na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia kifo.
Wankyo alisema Polisi walimkamata mtuhumiwa huyo na anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Tumbi huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea. Kuhusu chanoz cha tukio hilo, kamanda huyo alisema uchunguzi wa kujua ni nini kilitokea bado unaendelea.
Gazeti la UWAZI lilizungumza na ndugu, majirani na wanafunzi ambapo kila mtu alionesha kuwa na sintofahamu ya kutoamini kilichotokea kwa wanandoa hao kwani ni tukio ambalo halikutegemewa.
Watu hao walimtaja Mwalimu Joyce kama mtu mzuri mno kwani muda mwingi anakuwa na furaha na haijawahi kusikika kama ana mgogoro wa kindoa na mumewe huyo.
Kwa upande wake, kaka wa askari huyo aliyejitambulisha kwa jina la Enock Warioba alikuwa na haya ya kusema juu ya tukio hilo;
“Hatukuwahi kujua au hata kusikia kama kuna ugomvi.
“Ni kweli hili tukio limeibua sintofahamu maana kila mtu ameshtuka.
“Hakuna aliyetegemea kama lingetokea jambo baya na la kutisha kama hili.
“Tunapata utata kwa sababu wa kumuuliza hayupo ili tujue kisa ni nini hasa, lakini ndiyo hivyo mmoja ameshafariki dunia na yule aliyepo hospitalini, labda atakayeruhusiwa kuzungumza naye hospitalini ndiye anaweza kueleza kwa kina.”
Naye jirani wa wanandoa hao aliyejitambulisha kwa jina la Mama Neema alisema;
“Sijawahi kusikia kama wana ugomvi. Hili tukio la kikatili ambalo jamii yoyote haiwezi kulifurahia kwa kweli kwani linatisha.
“Ilikuwa ni nyumba yenye amani na utulivu. Ni tukio ambalo limeumiza wengi na kuacha maswali kwa kila mtu.”
Mwandishi Wetu, Uwazi
GPL