Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amekemea suala la wananchi kununua bidhaa bila kupewa risiti huku pia akiiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwashughulikia wafanyabiashara wanaohujumu uchumi kwa kutoa risiti za uongo.
Magufuli ameyasema hayo Disemba 28 alipokuwa akiongea na wananchi wa Mwanza katika eneo la Kigongo-Busisi, muda mfupi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2.
''Wananchi mnatakiwa kulipa kodi ili hii miradi ifanyike, hakikisha unachukua risiti kwa kila bidhaa unayonunua na muuza duka pia atoe risiti ambayo hela yake amepokea. Kumekuwa na tabia muuzaji anauza bidhaa ya milioni mbili yeye anatoa risiti ya elfu mbili, nimeagiza TRA hao wote washughulikiwe kwasababu wanahujumu miradi kama hii'', alisema Rais Magufuli.