BAADA ya kutua Simba, kiungo mpya wa timu hiyo, Taddeo Lwanga amepewa program maalum na kocha wake, Sven Vandenbroeck ili kuhakikisha anakuwa fiti zaidi.
Lwanga raia wa Uganda, amesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili baada ya mchezaji huyo kuwa huru ikiwa ni muda mchache tangu atoke kuvunja mkataba na timu yake ya Tanta FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.
Amepewa jezi namba nne iliyokuwa inavaliwa na kiungo mkabaji Gerson Fraga raia wa Brazil ambaye kwa sasa anatibu jeraha la goti.
Jumatatu ya wiki hii, Lwanga alianza mazoezi na kikosi cha Simba, ambapo katika mazoezi ya Jumanne yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena, Dar, alionekana akikimbia tu mwanzo mwisho bila ya kugusa mpira kama wenzake.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwa takribani saa 1:30 na kushuhudiwa na Spoti Xtra, wakati yeye akiwa na progamu yake maalum ya kukimbia pekee kwa muda huo, wachezaji wengine wa Simba waliendelea na program za ndani ya uwanja ikiwa pamoja na kuchezea mpira.