Mbunge wa India atishia kumpatia talaka mkewe aliyehamia chama pinzani




Uhusiano wa muda mrefu wa wanandoa wanasiasa katika jimbo la India la West Bengal umegonga mwamba huku vichwa vya habari vikisema kwamba mume ametishia hadharani kumpatia talaka mkewe baada ya kuhamia chama pinzani.

Siku ya Jumanne Saumitra Khan , mbunge kutoka chama cha waziri mkuu Narendra Modi cha Bharatiya Janata BJP alituma ilani ya talaka kwa mkewe Sujata Mondal Khan, siku moja baada ya kujiunga na chama cha Jimbo hilo Trinamol Congress Party TMC.

Jimbo la West Bengal linajiandaa kwa uchaguzi mdogo katika kipindi cha miezi michache na kinyanganyiro kikuu ni kati ya BJP na TMC.

Katika mkutano na waandishi wa habari katika mji wa jimbo hilo Kolkata , siku ya Jumatatu , bi Mondal Khan alitangaza uamuzi wake kukihama chama cha BJP huku akitoa sababu kadhaa za hatua yake.

 Alisema kwamba chama hicho hakikumpa heshima na kwamba kiliwakaribisha viongozi kadhaa wafisadi kutoka vyama vingine na kuahidi kuwazawadi bila ya kutilia maanani wanachama watiifu.

''Chama cha BJP kimekuwa Trinamol ndogo . Hivyobasi kwanini nisalie katika chama hicho? Kwanini nisiende katika timu kubwa ya Trinamol TMC''? , alisema.

Saa chache baadaye, katika mkutano ulioitishwa kwa haraka, ambao waandishi wa habari waliutaja kuwa uliokumbwa na viroja, bwana Khan mwenye umri wa miaka 40 alizuia machozi huku akionesha uchungu wake na kutoa hasira wakati akitangaza uamuzi wake wa "kukata uhusiano wa miaka 10" na mkewe.

Alimuomba mkewe kufuta jina lake la mwisho .

''Tafadhali usiendelea kutumia jina la 'Khan', tafadhali usijiite Saumitra Khan. Nakupatia uhuru wako wote uendelee na siasa yako, chombo cha habari cha Press Trust of India kilimnukuu akisema. Baadaye aliendelea kusema '' TMC kimemuiba mke wangu , kimeiba penzi langu.

Mwanahabari mkongwe kabisa katika jiji hilo alisema ilikuwa "mchezo wa kuigiza wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa hapo awali" na hadithi ya ndoa inayokwisha, iliyochezwa kwenye vituo vya habari vya Runinga, imeamsha watu.

Tangu mikutano ya waandishi wa habari Jumatatu, wawili hao walitafutwa na waandishi wa habari na walitoa mahojiano kadhaa - ya kibinafsi na ya kisiasa yanayoingiliana.

"Alikuwa mpenzi wangu. Alikuwa mke mzuri sana. Alikuwa udhaifu wangu pekee. Kwa kweli, nina hisia. Tulikuwa pamoja kwa miaka 10," Bwana Khan alimwambia mwandishi wa habari mmoja.

Alikubali jukumu la mkewe katika ushindi wake wa uchaguzi mwaka jana - alizuiliwa kuingia katika eneo bunge lake na korti kuhusiana na kesi ya jinai na alikuwa amefanya kampeni nyingi kwa niaba yake, akienda nyumba kwa nyumba akiomba kura na kutembelea vijiji vya mbali kutoa hotuba.

"Lakini muda wetu umeisha. Sina uhusiano wowote naye," alisema. "Nimekubali - Sujata hayupo tena kwangu."

Kwa mwandishi mwengine, alipuuza madai ya mkewe kwamba hakuheshimiwa katika BJP. "Bwana Modi anamwita kama dada yake. Anaweza kuomba nini zaidi?" Aliuliza.

Aliwashutumu viongozi wa BJP kwa "kumchochea" mumewe na kujaribu "kuharibu ndoa yake".

"Nani amesema kwamba Soumitra anatishia kuniacha?" Aliuliza vyombo vya habari akijaribu kuzuia machozi kutiririka.

Wanasiasa kuhamia vyama vingine sio jambo la kawaida nchini India. Na kwa kweli hawapaswi kumshangaza Bwana Khan - alianza kazi yake katika chama cha Congress, akahamia TMC mnamo 2013 na akajiunga na BJP mnamo Januari 2019 tu.

Pia, haijulikani kwa wapinzani wa kisiasa kukaa pamoja. Huko India, na ulimwenguni kote, kuna matukio ya wanafamilia wanaounga mkono vyama pinzani na ndoa zenye furaha katika uwanja wote wa kisiasa.

Huko Bengal pia, kama vile Bi Mondal Khan ameonyesha, wanasiasa kadhaa wa eneo hilo - baba na wana, wajomba na kaka - ambao wanaunga mkono vyama vivyopingana kabisa "wanaishi kwa furaha na hakuna mtu anayewaambia waachane".

"Ni njama ya BJP, wanamwomba aachane nami," alimwambia mmoja aliyemuhoji. "Lakini nadhani siasa na nyumba ni tofauti na zinapaswa kuwekwa kando."

Bi Mondal Khan pia alivunjika moyo katika mahojiano wakati alimshtumu mumewe kwa kumpuuza kwa miezi 10 iliyopita.

"Amekuwa akijishughulisha na siasa. Hana muda na mimi. Kwa miezi, hajajisumbua kuuliza ikiwa nimekula au nimelala vipi," alisema.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad