WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameagiza watumishi 22 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Amesema wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kujihusisha na ufisadi na kuikosesha Serikali mapato na kumtaka kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Edwin Mhede kuwasimamisha kazi.
Amebainisha kuwa watu hao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutosimamia ipasavyo matumizi ya mashine za kutolea stakabadhi (EFD’s), kuwabambikia kodi kubwa wafanyabiashara na kuagiza apatiwe taarifa ya utekelezaji wa maelekezo yake ndani ya siku 90 kuanzia leo.
Ametoa maagizo hayo leo Jumatano Desemba 16, 2020 mjini Dodoma katika kikao kilichozihusisha bodi za wakurugenzi, menejimenti na mameneja wa mikoa wa mamlaka hiyo.
Lengo la kikao hicho lilikuwa kupanga mikakati namna ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali.
“Nakuagiza kamishna mkuu uwapumzishe kazi kuanzia leo kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 na umwagize mkuu wa idara ya mambo ya ndani awachunguze wahusika wote ndani ya siku 90 na nipatiwe nakala ya taarifa hiyo ya uchunguzi na hatua zilizochukuliwa dhidi ya kila mmoja wao,” amesema.