WIZARA ya mazingira ya Namibia imesema kwamba serikali ya nchi hiyo inapanga kuuza ndovu (tembo) 170 kutokana na hali mbaya ya kiangazi na idadi kubwa ya ndovu katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Tangazo la kuuzwa kwa ndovu hao limetolewa na shirika la habari la serikali la New Era ambalo limeripoti kuongezeka kwa visa vya ndovu kushambulia binadamu na ndovu hao kuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na uwindaji haramu pamoja na sababu za kimazingira.
Wizara ya mazingira, misitu na utalii imesema kwamba itauza ndovu hao kwa mnada kwa mtu yeyote ndani ya Namibia au nje ya nchi chini ya mpangilio maalum utakaowekwa kuhusu mahali ndovu hao watawekwa iwapo wananunuliwa na mtu ndani ya nchi.
Raia wa nchi nyingine wanaotaka kununua ndovu hao, wanatakiwa kuonyesha idhini ya maafisa nchini mwao kwamba wanaruhusiwa kuingiza ndovu hao nchini mwao.
Idadi ya ndovu imeongezeka kwa kasi nchini Namibia, kutoka 7,500 mwaka 1995 hadi 24,000 mwaka 2019.