Ndugai awaita wabunge wa ACT-Wazalendo bungeni

 


Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewaita wabunge wanne wa ACT-Wazalendo akiwataka kutoa taarifa za kuripoti bungeni ili awapangie tarehe ya kuapishwa.


 Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 11, 2020 katika viwanja vya Bunge wakati akimwapisha mbunge wa kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya.


Kuapishwa kwa Profesa Manya kunafanya idadi ya wabunge walioteuliwa na Rais kufikia watano.


Profesa Manya aliteuliwa kuwa mbunge na naibu waziri wa madini baada ya aliyeteuliwa awali, Francis Ndulane kushindwa kusoma kiapo chake mbele ya Rais John Magufuli.


“Natoa wito kwa wabunge wanne wa ACT Wazalendo watoe taarifa zao mapema na tuwapangie tarehe ya kuapishwa kama kweli wana nia ya kuitumikia nchi yao kama walivyoomba kwa wananchi badala ya kuendelea kuzurura huko,” amesema  Ndugai.


Tofauti na siku zote, leo Ndugai alitumia dakika moja kuzungumza akisisitiza mbunge huyo kulitumikia Bunge kwa uadilifu kama alivyoaminiwa na Rais na kupitia nafasi adhimu ambazo hutolewa na kuomba amtangulize Mungu katika utumishi wake.


 Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Profesa Manya amesema  hakutegemea kushika nafasi hiyo bali Mungu ndiye mgawaji wa kila jambo kwa watu wake.


Profesa Manya amesema Mungu anajua kupanga majira na nyakati zake kwamba hapa afanye nini na kwa wakati gani, kuahidi kufanya kazi kwa uadilifu ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo huku akiomba kumtanguliza Mungu.


Waziri wa Madini, Dotto Biteko alimweleza Profesa Manya kuwa wachimbaji madini wadogo wanahitaji maeneo ya kuchimba madini pamoja na kupatiwa mikopo ili wafanye kazi zao kwa uhakika zaidi.


Waziri Biteko amesema juzi baada ya uteuzi alimwita Profesa Manya na kuzungumza naye ofisini kwake ambapo alimwambia matarajio ya Rais katika Wizara hiyo akisema kwa sasa lazima Serikali ifanye utafiti wa kutosha kabla ya kuwapa maeneo wachimba.


Kuhusu watu wanaotorosha madini amesema wanataka vitu viwili ambavyo ni umasikini ama kwenda jela hivyo akaonya waache kufanya kazi hizo mara moja.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad