RATIBA ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Ihefu FC dhidi ya Yanga uliotarajiwa kuchezwa Desemba 26, imepanguliwa na kurudhishwa nyuma.
Wakiwa wametoka kumalizana na Dodoma Jiji, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jana Desemba 19 watakuwa na kazi ya kumenyana na Ihefu FC, Uwanja wa Sokoine Desemba 23.
Mabadiliko hayo yametokana na mechi za raundi ya tatu za michuano ya Kombe la FA ambapo Yanga inatarajiwa kucheza na Singida United kati ya Desemba 25 na 27.
Tayari kikosi cha Yanga kimeondoka mkoani Arusha kuanza safari kuelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Ihefu FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Zuber Katwila.
Akizungumza na Saleh Jembe, Meneja wa Yanga Hafidh Saleh amesema wapo tayari kwa mchezo huo na watatumia Uwanja wa Sokoine kwa kuwa Yanga ni timu ya Wananchi na ina mashabiki wengi kila kona.
“Tunajua kwamba Ihefu wana Uwanja wao ule wa Highlands ila hautatutosha sisi ukizingatia kwamba ni timu kubwa na ina mashabiki wengi huu ni ukweli.
“Kila kitu kipo sawa mashabiki watupe sapoti ili tuendelee kufanya vizuri ndani ya uwanja,” .
Yanga kwenye msimamo ipo nafasi ya kwanza ina pointi 40 baada ya kucheza mechi 16 haijapoteza mchezo ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21.