Mkuu wa mkoa wa Mbeya Albert Chalamila, amesimamia zoezi la kubomoa nyumba ya Atony Lyuba mkazi wa Kata ya Inyala, Halmshauri ya wilaya ya Mbeya, baada ya kukaidi agizo la kubomoa kwa hiari nyumba yake.
Uamuzi wa RC Chalamila, ulitokana na Lyuba kukaidi agizo la kupisha mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 16.7, ambao unajegwa kwa kiwango cha lami kuanzia Inyala hadi eneo la Simambwe, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali walifika kumtaka avunje nyumba yake kwa hiari lakini aligoma.
"Nimeamua nije mwenyewe kubomoa nyumba yako, maana kila wakati tulikuomba kwa hiari yako lakini uligoma, haiwezakani wenzako wote wakubali kubomoa halafu wewe peke yao ugome kama ni Imani za kishirikinabasi tutaziona", amesema Chalamila.
Mkandarasi wa mradi huo, Imelda Ngailo, amesema kuwa kugoma kubomoa kwa nyumba hiyo kumechelewesha kuendelea na shughuli kwa sababu ya nyumba yake kuwa katikati ya hifadhi ya barabara na kwamba mradi huo ulitakiwa ukamilike Desemba mwaka huu lakini utachelewa kutokana na kikwazo hicho.
Akizungumza na EATV kuhusu suala ya kukaidi kubomoa nyumba yake, Antony Lyuba, alikanusha madai ya yeye kugoma kubomoa nyumba na kwamba hakuna kiongozi yeyote alimfuata kumpa maelekezo.
"Hakuna Mwenyekiti wa Kijiji wala Kata aliyekuja kwangu kuniambia nibomoe nyumba, zaidi ya kufika ofisini kwako mkuu wa mkoa na nikaamuriwa kuwa niko chini ya ulinzi kwa kukaidi agizo la kubomoa kwa hiari nyumba yangu," amesema Lyuba.