Mamia ya wanafunzi ambao walitekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram kutoka shule ya bweni katika jimbo la Katsina nchini Nigeria, wamebainishwa kuzuiwa katika msitu wa jimbo jirani la Zamfara.
Gavana wa jimbo la Katsina Aminu Masari, aliarifu kujadiliana na kundi hilo kwa ajili ya kuachiliwa kwa wanafunzi hao, na kusema,
"Tunafanya mazungumzo kupitia idara yetu ya usalama wa eneo hilo, lakini haturuhusu mjadala wa pesa. Kama gavana wa jimbo, nina jukumu la kuokoa wanafunzi 402 ambao wamepotea."
Wanamgambo wa Boko Haram walishambulia shule ya bweni kwenye wilaya ya Kankara katika jimbo la Katsina usiku wa Desemba 11, na kuwateka nyara zaidi ya wanafunzi 500.
Gavana wa Katsina Masari aliamuru "shule zote za bweni katika jimbo hilo zifungwe" baada ya mashambulizi hayo.
Waziri wa Ulinzi wa Nigeria Bashir Salihi Magashi, alitembelea eneo hilo na kuahidi kuwa wanafunzi wataokolewa haraka iwezekanavyo.
Rais Mohammed Buhari alishutumu shambulizi hilo la woga dhidi ya watoto wasio na hatia lililoendeshwa na kundi hilo la silaha na kusema kwamba vikosi vya usalama vimegundua maficho ya msituni ya kundi hilo kwenye operesheni iliyoanzishwa.
Msemaji wa Polisi wa Jimbo la Katsina Gambo Isah, pia alisema kuwa afisa mmoja wa usalama alijeruhiwa wakati wa operesheni hiyo, na kutuma maafisa zaidi wa vikosi vya usalama kusaidia shughuli ya utafutaji na uokoaji.