Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mchana vya malezi ya watoto Mkoani Arusha kurekebisha kasoro zilizopo kabla vituo hivyo havijafungiwa.
Dkt. Jingu ametoa agizo hilo alipotembelea baadhi ya vituo katika jiji la Arusha, kikiwemo kituo cha Leonason, na kutoridhishwa na uendeshaji wake baada ya kubaini vituo hivyo kutozingatia masharti ya kutoa huduma hiyo ikiwemo maeneo finyu na kuagiza wamiliki wake kutafuta maeneo mengine.
“Eneo hili halikidhi mazingira ya kuwa kituo cha malezi ya watoto mchana kwa hiyo nawapa wiki mbili mrekebishe yote, mtafute eneo jingine, maafisa ustawi waje kufanya ukaguzi,baada ya siku 14 kama mtakuwa hamjakidhi tutakifunga” amesema Dkt. Jingu
Aidha Dkt. Jingu amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii Jijini hapo, kukagua vituo vya malezi ya watoto mchana mara kwa mara kwani kutokana na ukaguzi alioufanya amebaini maafisa hao hawatembelei vituo hivyo hivyo haviendeshwi kulingana na utaratibu.
Kwa upande wao baadhi ya wasimamizi wa vituo vilivyotembelewa wamekiri vituo hivyo kuendeshwa kinyume na utaratibu ikiwemo kutokuwa na usajili pamoja na mazingira yasiyofaa kwa malezi ya watoto wadogo na kuahidi kurekebisha kasoro hizo.
Wizara ya Afya kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inaendelea na ukaguzi wa vituo vya malezi ya watoto mchana huku baadhi ya vituo vikifungiwa kutokana na kuendeshwa kinyume na utaratibu.