LICHA ya Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Plateau United, lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amelitaka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitia upya vigezo vilivyotumika kuruhusu mchezo wao huo kuchezwa kwenye Dimba la New Jos, Nigeria.
Kiongozi huyo ameweka bayana kuwa uwanja huo ambao ulitumika kwenye mchezo wa awali haujakidhi viwango vinavyohitajika.
Wikiendi iliyopita, Simba ikiwa ugenini, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wikiendi hii jijini Dar, Desemba 5.
Barbara alisema kwenye kanuni na taratibu za CAF zinaelekeza aina gani ya uwanja unaotakiwa kupewa leseni ya kuchezewa michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kama vile ubao wa kieletroniki kwa ajili ya kuonyesha matokeo, dakika na vitu vingine muhimu ambavyo Uwanja wa Jos hauna.
Akiuzungumzia uwanja huo, Barbara amesema:- "Kuna mapungufu mengi sana ambayo uwanja wa Jos unafanya ukose sifa ya kupewa leseni ya kutumika katika michezo ya kimataifa. Kanuni za CAF zipo wazi, lazima uwanja uwe na eneo bora la kuchezea, vyumba vya kubadilishia nguo, ubao wa 'electronic' na vitu vingine vingi ambavyo uwanja huu wa umekosa.
"Sasa CAF inabidi waweke wazi na watuambie ni vigezo gani ambavyo vilitumika hadi kuruhusu na kutoa kibali kwa Uwanja wa Jos kutumika kwa michezo ya kimataifa." amesema.
Bao la ushindi lilifungwa na Clatous Chama dakika ya 53 kwa pasi ya Luis Miqussone ambao wote ni viungo wa kigeni.