Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Geogre Simbachawane amewataka Watanzania kutunza amani iliyopo nchini na pia kuenzi misingi ya maadili mema yaliyoachwa na Waasisi wa Taifa.
Amesema amani na upendo uanzia katika familia, hivyo katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi familia zinajenga upendo na amani, hivyo amani hiyo iwe pia katika kujenga Taifa.
Simbachawene amezungumza hayo katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria wa Rozali Pwaga, Jimbo la Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, leo, ambapo mamia ya waumini walihudhuria misa hiyo, ambayo pia iliombwa na familia ya Marehemu Mzee Simbachawene wakiwaombea marehemu mbalimbali wa ukoo huo.
“Familia ziishi kwa upendo, kushirikiana, kusameheana, kupendana, kuwa na amani, hivyo familia zinapoungana zinaunga jamii, na zinajenga upendo ndani ya taifa, kila mtu achukue nafasi yake katika familia yake ili tuweze kujenga taifa,”alisema Simbachawene.
Pia Waziri Simbachawene amesem, mwaka 2020 unaishia nchi imepitia katika matukio makubwa hata hivyo nchi imebaki salama, matukio hayon ni ugonjwa wa corona lakini nchi imebaki salama, pia uchaguzi mkuu umemalizika ukiwa wa huru na amani, hivyo hatua zote hizo tunapaswa kumshukuru Mungu kwa taifa kuvushwa salama.
“Nchi mpaka sasa ipo salama, dunia imepigwa na corona, lakini sisi Tanzania tupo salama, tumepita katika uchaguzi mkuu umeisha salama, uchaguzi haukosagi kelele, hata Marekani kuna kelele, wao wameendelea na ndiuo taifa kubwa duniani, na hata walipomaliza uchaguzi kelele hazikosekani, hata sisi kulikua na kelele lakini hatukuvunja taifa, lakini tumepita salama tunamshukuru Mungu,” alisema Simbachawene.
Pia Simbachawene amewataka madereva wa vyombo vya moto hasa bodaboda kuwa makini barabarani hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, wawe makini wasije leta vilio katika familia mbalimbali kutokana na kutokea kwa ajali.
“Kuna upungufu mkubwa sana wa hali ya ajali nchini kwa miaka mitano iliyopita mpaka sasa, mwaka 2017 kiwango cha ajali ilikuwa 9,250, lakini tangu januari mpaka novemba mwaka huu ajali zimekuwa 1,602 hii kwasababu wananchi wanaendelea kufuata sheria za usalama barabarani lakini pia asakri polisi, kitengo cha trafiki wamefanya kazi vizuri, kuhakikisha wanaendelea kudhibiti ajali,” alisema Siumbachawene.
Aidha, Waziri Simbachawene amechangia shilingi milioni tano ikiwa ni kwz ajili ya ukoo wa Mzee Simbachawene kijijini hapo, na kuwataka waumini wafanye kazi ili waweze kupata fedha na kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.
Kwa upande wake Kaimu Paroko wa Kanisa hilo, Padri Stephen Umondi amempongeza Waziri huyo kwa kuchangia fedha za ujenzi wa kanisa hilo, na linatarajia kuanza kujengwa mwaka 2021 ambapo litakua kanisa kubwa katika Wilaya ya Mpwapwa.
“Tunakushuru sana mgeni wetu kwa kutoa shilingi milioni tano, tayari michoro ipo tayari, na ipo kwa baba askofu mkuu na anaramani mbili, ambao atachagua moja ipi ijengwe, na kanisa litakalojengwa mwakani litakua kubwa kuliko yote hapa Mpwapwa, na pia kanisa hilo litakua na uwezo wa kubeba waumini 600 hadi 800,” alisema Padri Umondi.